Sep 24, 2020 11:32 UTC
  • Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini
    Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini

Mabadiliko ya kimsingi katika muundo wa mfumo wa kimataifa na kuongezeka nafasi ya maeneo mbalimbali ya dunia ikiwemo Afrika vimezidisha maombi ya nchi muhimu za bara hilo zikitaka kuzidishwa nafasi ya uwakilishi wa Afrika katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ambaye ni Mwenyekiti wa kiduru wa Umoja wa Afrika (AU) amesema kuwa nchi za Afrika zinapasa kuwa na wawakilishi zaidi katika Baraza la Usalama na kwamba suala hilo lizingatiwe kwenye mazungumzo baina ya serikali mbalimbali.

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini  

Amesisitiza kuwa ni kupitia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililofanyiwa marekebisho na lenye kuzishirikisha pande mbalimbali ndipo tunaweza kuyapatia suluhisho mapigano ya muda mrefu duniani.  Rais Ramaphosa ametoa wito huo alipohutubia mkutano wa 75 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa njia ya video juzi Jumanne. Msimamo huu wa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika juu ya ulazima wa kufanyiwa marekebisho muundo wa sasa wa Baraza la Usalama unapata maana zaidi kwa kuzingatia mabadiliko yaliyotokea katika ngazi ya kimataifa na kujitokeza nguvu kubwa mpya za kiuchumi na pia kuongeza nafasi ya Afrika katika uwanja wa kimataifa. 

Sayyid Muhammad Marandi ambaye ni mchambuzi wa masuala ya kimataifa anaamini kuwa: Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lina muundo wa unaopendelea upande mmoja na usio wa kiadilifu, na ili kubadilishwa muundo huo kuna ulazima wa kuanzishwa taasisi mabadala.  

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lina wanachama watano wa kudumu na kumi na tano wasio wa kudumu. Wanachama 5 wa kudumu wa baraza hilo wana na haki ya kura ya veto. Mara ya mwisho muundo wa Baraza la Usalama ulifanyika mabadiliko mnamo mwaka 1965 kwa kuzidishwa nchi 11  na kuwa na wanachama 15. Hata hivyo, wakati huo idadi ya wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama ambao walikuwa na haki ya kupinga maamuzi ya taasisi hiyo kwa kutumia kura ya veto haikubadilika. Nchi wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama ni Marekani, Russia, China, Uingereza na Ufaransa. 

Baraza la Usalama la UN   

Kuanzia miaka 75 iliyopita wakati Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipoasiwa kwa kile kilichotajwa kuwa ni kwa ajili ya kulinda usalama duniani hadi sasa, hakuna mabadliko yoyote makubwa yaliyoshuhudiwa ndani ya taasisi hiyo au kufanyiwa marekebisho muundo wake licha ya mabadiliko makubwa yaliyoikumba duniani katika kipindi chote hicho. Naam, kumeshuhudiwa mabadiliko kadhaa madogo katika taasisi hiyo muhimu ikiwa ni pamoja na kuongezwa idadi ya wanachama wa kuchaguliwa kutoka nchi 6 na kufikia 10, na Russia kupatiwa kiti cha kudumu ndani ya baraza hilo na haki ya kura ya veto baada ya kusambaratika Umoja wa Kisovieti. Hii ni katika hali ambayo baadhi ya mabara na maeneo ya dunia hayana mwakilishi yoyote wa kudumu ndani ya Baraza la Usalama. Kwa mfano bara la Afrika halina mwakilishi wa kudumu katika baraza hilo licha ya kuwa na nchi 53. Eneo la Asia na Pacific lina mwanachama moja tu yaani China katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa licha ya kuwa na nchi 56. Bara la Ulaya ambalo lina nchi 48 linawakilishwa na nchi tatu wanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama ambazo pia zina haki ya kura veto. Katika bara la Amerika pia ni Marekani tu ndio mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama. Nchi za Ulimwengu wa Kiislamu pia hazina mwanachama yoyote wa kudumu katika Baraza la Usalama. 

Bara la Afrika halina mwakilishi yoyote wa kudumu katika Baraza la Usalama 

Hii ni katika hali ambayo baada ya kuundwa kundi la G-20 linalozijumisha nchi zilizoendelea na zile zinazostawi kiuchumi, aghalabu ya nchi za kundi hilo kama Japan, Afrika Kusini, Brazil na Ujerumani zimetaka kufanyiwa marekebisho muundo wa Baraza la Usalama. Nchi hizo zinaamini kuwa, kutokana na mabadiliko yaliyotokea katika ngazi ya kimataifa na umuhimu mkubwa wa baadhi ya nchi katika sekta ya kiuchumi na kisiasa katika ngazi ya kimataifa, kuna udharura wa kufanyika mabadiliko pia katika Umoja Mataifa hususan katika Baraza la Usalama la umoja huo, na idadi ya wanachama wa kudumu wa baraza hilo ibadilishwe.

Inaonekana kuwa, licha ya wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama kupinga, kwa sababu zao makhsusi, uwepo wa wanachama wapya wa kudumu ndani ya baraza hilo, lakini hali halisi ya kimataifa hatimaye italazimisha kufanyika mabadiliko katika muundo wa sasa wa Baraza la Usalama na kutoa nafasi ya kuwepo wanachama wapya wa kudumu katika baraza hilo zikiwemo nchi za bara la Afrika.  

Tags

Maoni