Sep 24, 2020 12:01 UTC
  • Umoja wa Mataifa: Zaidi ya watu 1,800 wameuawa Ituri, DRC katika miezi ya karibuni

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, zaidi ya watu 1,800 wameuawa katika mkoa wa Ituri uliopo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika miezi ya hivi karibuni huku wengine karibu milioni mbili wakilazimika kuyakimbia makazi yao.

Mbunge Jackson Ausse ameiambia Radio ya Umoja wa Mataifa kwamba, katika kipindi mauaji hayo yametokea katika kipindi cha miezi sita iliyopita katika mkoa huo na kwamba, shule zisizpungua 300 zimeharibiwa kufuatia machafuko na mapigano mkoani humo.

Mbunge huyo amemtaka Rais Felix Tshisekedi kutangaza hali ya dharura ya usalama katika mkoa wa Ituri na vile vile katika mkoa wa Kivu Kaskazini maeneo ambayo kwa sasa yanakabiliwa na hali mbaya ya ukosefu wa usalama kutokana na harakati za makundi ya wanamgambo katika mikoa hiyo.

Hayo yanajiri wakati ambapo mapigano ya kikabila katika mkoa wa Kasai huko huko katika  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, yamesababisha vifo vya watu 11 na wengine zaidi ya 10,000 kuyakimbia makazi yao huku nyumba zaidi ya 1,000 zikiteketezwa moto, katika mapigano yaliyotokea mapema mwezi huu.

Wapiganaji wa ADF moja ya makundi ya wanamgambo yanayoendesha harakati zake mashariki mwa DRC

 

Eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo  limekuwa likishuhudia machafuko ya mara kwa mara baina ya makundi ya wanamgambo kwa upande mmoja na wanamgambo na maafisa usalama kwa upande mwingine, kutokana na kuwa na utajiri mkubwa wa madini hususan dhahabu na almasi. 

Mashirika mbalimbali ya utoaji misaada ya kibinadamu yamekuwa yakionya kuhusiana na hali mbaya ya kibinadamu katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo na kutoa wito wa kukomeshwa machafuko.

Maoni