Sep 24, 2020 12:02 UTC
  • Botswana sasa kuanza kutumia lugha ya Kiswahili mashuleni

Serikali ya Botswana imetangaza kuwa, inakusudia kuanza matumizi ya lugha ya Kiswahili katika Shule za Msingi za nchi hiyo ya Kiafrika.

Hayo yameelezwa na Fidelis Molao Waziri wa Elimu ya Msingi wa nchi hiyo ambaye amebainisha kuwa, matumizi ya lugha ya Kiswahili yataanzishwa katika shule za Botswana ndani ya siku chache zijazo.

Waziri huyo amesema kuwa, maandalizi yote ya kuanza kufundisha lugha ya Kiswahili katika shule za nchi hiyo yamekamilika. Waziri Molao amesema, Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) itakuwa na washirika wakubwa wa kibiashara na nchi nyingi zinazozungumza Kiswahili katika siku za usoni jambo ambalo hata Botswana inalihitaji zaidi katika kukuza uchumi na mauzo ya nje. 

Kiswahili ni lugha ya Kibantu inayozungumzwa sana katika eneo la Maziwa Makuu na sehemu zingine za Mashariki na Kusini Mashariki mwa Afrika ikiwa ni pamoja na Kenya, Tanzania, Burundi, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na sehemu za Malawi.

 

Ikiwa Kiswahili kitatumika Botswana itakuwa ni lugha ya kwanza ya Kiafrika kutumika kutoka nje ya mipaka ya nchi hiyo ambayo ni mzalishaji mkubwa wa Almasi Ulimwenguni.

Weledi wa mambo wamekuwa wakisema kuwa, Kiswahili ni lugha ya aina yake ambayo inaweza kutumika katika nchi zote za bara Afrika, kama njia moja ya kuliondoa bara hilo kutoka katika minyororo ya ukoloni mambo leo.

Maoni