Sep 25, 2020 03:06 UTC
  • Amnesty yaitaka EU kushirikiana na Libya katika faili la wahajiri

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeutaka Umoja wa Ulaya (EU) kutazama upya ushirikiano wake na maafisa wa serikali ya Libya katika faili la makumi ya maelfu ya wahajiri walioko nchini humo.

Ripoti iliyotolewa jana na Amnesty International imeeleza masikitiko yake kutokana na sera za Umoja wa Ulaya mkabala wa wahajiri na wakimbizi walioko Libya na kusema kuwa: Umoja wa Ulaya na nchi wanachama wake zinatekeleza sera na siasa zisizofaa dhidi ya makumi ya maelfu ya wahajiri na wakimbizi ambazo zinakanyaga waziwazi maisha na ubinadamu wao. 

Amnesty International imesema katika ripoti hiyo iliyotolewa kwa anwani ya "Baina ya Mauati na Uhai" kwamba, wakimbizi na wahajiri walioko Libya wako kwenye mzingiro wa maumivu makali ya ukiukaji wa haki za binadamu. 

Wahajiri wa Kiafrika nchini libya

Ripoti hiyo imesisitiza kuwa, wahajiri walioko Libya wanakabiliwa na mauaji, utekaji nyara, vitendo vya kunajisiwa, mateso, mienendo mibaya, kuwekwa kizuizini na kufanyishwa kazi la kulazimishwa. Makumi ya malfu ya wahajiri kutoka nchi mbalimbali wanasumbuliwa na matatizo mengi katika maeneo kadhaa ya Libya.

Miaka miwili iliyopita pia Amnesty International ilizituhumu nchi za Ulaya hususan Italia kuwa zinashirikiana na serikali ya Libya kuwatesa wakimbizi nchini humo. Baadhi ya vyombo vya habari vimetangaza kuwa wahajiri wa Kiafrika waliopo Libya wanauzwa kama watumwa kwa kiasi cha dola 400. 

Maoni