Sep 25, 2020 11:15 UTC
  • Jeshi la Nigeria ladai kuwaangamiza makamanda kadhaa muhimu wa Boko Haram

Jeshi la Nigeria limetangaza kuwa, limewaua makamanda kadhaa muhimu wa ngazi za juu wa kundi la kigaidi la Boko Haram katika operesheni kubwa ya jeshi hilo katika jimbo la Borno lililoko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Taarifa ya jeshi la Nigeria ambayo haikutaja idadi ya makamanda hao imedai  kuwa, miongoni mwa makamanda hao wa ngazi za juu wa Boko Haram waliouawa ni pamoja na Abu Usman, Alhaji Shettima, Modu Mainok, Bukar Gana, Abu Sumayya, Amir Taam na Amir Kuraish.

Kadhalika taarifa ya jeshi la Nigeria imeeleza kuwa, kambi kadhaa za wanamgambo wa kundi la kigaidi la Boko Haram zimeharibiwa kabisa katika eneo moja jirani na Ziwa Chad.

Wiki iliyopita pia, jeshi la Nigeria lilitangaza habari ya kuuawa wanachama 16 wa kundi la kigaidi la Boko Haram huko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram lilibeba silaha na kuanzisha uasi mwaka 2009 kwa lengo la kuasisi utawala eti wa Kiislamu kaskazini mwa Nigeria, ambapo mbali na ndani ya nchi hiyo, limepanua wigo wa mashambulio yake katika nchi jirani pia za Niger, Chad na Cameroon.

Wanamgambo wa Boko Haram wamefanya mauaji mengi ya kutisha nchini Nigeria na katika nchi za jirani

 

Zaidi ya watu 20 elfu wameuawa katika nchi hizo nne za magharibi mwa Afrika na zaidi ya wengine milioni mbili wamekuwa wakimbizi baada ya kulazimika kuyahama makazi yao.

Serikali ya Rais Muhamadu Buhari imeendelea kukosolewa kutokana na kushindwa kutekeleza ahadi zake alizotoa wakati wa uchaguzi ikiwemo ya kulitokomea kundi la kigaidi la Boko Haram ambalo limeendelea kufanya mauaji na kuhatarisha maisha ya raia hususan katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Maoni