Sep 26, 2020 12:21 UTC
  • Watu kadhaa wauawa katika maandamano ya kumtaka Rais wa Misri ajiuzulu

Kwa akali watu wawili wameuawa huku makumi ya wengine wakijeruhiwa katika ghasia za maandamano ya wananchi wa Misri, wanaomtaka Rais Abdel Fattah al Sisi wa nchi hiyo ang'atuke madarakani.

Maafisa usalama walitumia risasi hai na mabomu ya kutoa machozi kuzima maandamano hayo ya wananchi hapo jana, yaliyopewa jina la 'Ijumaa ya Ghadhabu.'

Mbali na mji mkuu Cairo, maandamano hayo yameshuhudia pia katika miji na mikoa mbalimbali ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika, kama vile Giza, Damietta katika jimbo la Nile Delta na Luxor, kusini mwa nchi. Waandamanaji walisikika wakipiga nara dhidi ya Rais wa nchi hiyo na kuwataka raia wote kujiunga na maandamano hayo ambayo hii leo yameingia siku ya saba.

Shirika la habari la Associated Press limenukuu duru za kiusalama zikiripoti kuwa, watu kadhaa wamekamatwa na maafisa usalama katika maandamano hayo yaliyogeuka na kuwa ya fujo jana Ijumaa, hususan jijini Cairo.

Rais wa Misri akihutubia askari wa nchi hiyo

Makundi na jumuiya mbalimbali za kisiasa zimeapa kwamba zitaendeleza maandamano hayo hadi Misri 'itakapokombolewa' kutoka kwenye mikono ya maghasibu wa utawala ambao wamesema wamelisaliti taifa, kulidhalilisha jeshi na kuitumbukia nchi katika mikataba ya kifisadi.

Tangu aliposhika madaraka ya nchi kupitia mapinduzi ya kijeshi hapo mwaka 2013, Abdel Fattah al Sisi amekuwa akikandamiza harakati zote za wapinzani wa serikali akiungwa mkono au kunyamaziwa kimya na nchi za Magharibi hususan Marekani.

Tags

Maoni