Sep 28, 2020 11:47 UTC
  • Wanachama 13 wa Boko Haram wajisalimisha kwa jeshi la Nigeria

Wanachama 13 wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Boko Haram wamejisalimisha kwa jeshi la Nigeria, katika operesheni iliyolenga kusafisha mabaki ya wanamgambo hao huko kaskazini mashariki mwa nchi.

Msemaji wa Jeshi la Nigeria, John Enenche alisema hayo jana Jumapili na kuongeza kuwa, watoto 17 na wanawake sita waliotambulishwa kama jamaa za magaidi hao wamejisalimisha pia katika operesheni hiyo iliyofanyika katika kijiji cha Kodila eneo la Baga, jimboni Borno.

Eneche ameongeza kuwa, kwa sasa washukiwa hao wanafanyiwa uchunguzi ili kujua namna kesi zao zitakavyoendeshwa kwa kuzingatia sheria za kitaifa na kimataifa.

Jeshi la Nigeria lilianzisha operesheni kali baada ya kundi hilo la kigaidi kufanya shambulizi la kuvizia dhidi ya msafara wa Gavana wa jimbo la Borno la kaskazini mashariki mwa Nigeria na kuua watu 30 wakiwemo maafisa usalama Ijumaa.

Silaha zilizokuwa mikoni mwa wanachama wa Boko Haram

Shambulizi hilo la Boko Haram lilijiri masaa machache baada ya jeshi la Nigeria kutangaza kuwa limewaua makamanda kadhaa muhimu wa kundi hilo la kigaidi katika operesheni kubwa ya jeshi hilo katika jimbo la Borno.

Zaidi ya watu 20 elfu wameuawa katika hujuma za Boko Haram tokea mwaka 2009 katika nchi nne za magharibi mwa Afrika za Nigeria, Niger, Chad na Cameroon, na wengine zaidi ya milioni mbili wamekuwa wakimbizi baada ya kulazimika kuyahama makazi yao kutokana na mashambulizi hayo.

 

Tags

Maoni