Sep 28, 2020 13:44 UTC
  • Tundu Lissu atakiwa na Tume ya Uchaguzi akajieleza kuhusu madai ya kuhujumiwa uchaguzi

Tume ya Uchaguzi nchini Tanzania (NEC) imemtaka Tundu Lissu mgombea wa urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA, kufika mbele ya kamati ya maadili ya Taifa kutoa ushahidi kuhusu madai aliyotoa dhidi yake.

Mkurugenzi wa Uchaguzi Dkt Charles Mahera amesema kuwa, Tume hiyo imesikitishwa na taarifa za uwongo, uzushi na upotoshaji zilizotolewa na mgombea wa urais wa upinzani Tundu Lissu siku ya Jumamosi, akisema kwamba Rais John Magufuli aliitisha kikao cha wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo yote nchi nzima mjini Dodoma kwa lengo la kuhujumu uchaguzi.

NEC imesema baadhi ya wagombea wamekuwa wakitumia maneno ya kukashifu wagombea wenzao, tume, pamoja na kutoa taarifa zisizo za kweli.

‘’Kitendo cha baadhi ya wagombea wa Rais hasa mgombea wa Chadema Tundu Lissu kuikashifu Tume kwamba itaiba kura zake ni kitendo cha kuidhalilisha Tume na kutaka kuitisha Tume ili isifanye kazi zake kwa uhuru’’ alisema Dkt. Mahera.

Rais John Pombe Magufuli

 

Hayo yanjiri katika hali ambayo, hivi karibuni Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch (HRW) lilitangaza kuwa, mamlaka nchini Tanzania imeongeza hatua za ukandamizaji dhidi ya vyama vya upinzani na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu hapo mwezi ujao.

Uchaguzi mkuu nchini Tanzania umepangwa kufanyika tarehe 28 ya mwezi ujao wa Oktoba na hivi sasa tayari kampeni za uchaguzi huo zinaendelea licha ya manung'uniko ya kambi ya upinzani kuhusiana na masuala mbalimbali kama kutokuweko tume huru ya uchaguzi, kutofanyika mabadiliko ya katiba na hata vyombo vya usalama kuonekana vinakipendelea chama tawala CCM.

Maoni