Sep 29, 2020 13:37 UTC
  • Magaidi wa al-Shabaab wavamia kambi ya AMISOM, kadhaa wauawa

Wanachama kadhaa wa kundi la kigaidi la al-Shabaab wameangamizwa katika operesheni mbili zilizojiri katika eneo la Lower Shabelle kusini mwa Somalia.

Kikosi Maalumu cha Danab cha Jeshi la Taifa la Somalia kimetangaza kuwa kimefanikiwa kuwaangamiza wanamgambo saba wa al-Shabaab na kuwajeruhi wengine kadhaa kwenye operesheni ya jana Jumatatu katika eneo la Lego mkoani Lower Shabelle.

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Somalia, Jenerali Yusuf Rageh Odowaa amesema vikosi vya nchi hiyo ya Pembe ya Afrika vitaendelea kushambulia ngome za kundi hilo la kigaidi hadi waangamizwe wote au wafurushwe katika eneo la Lower Shabelle.

Kundi la al-Shabaab limepata pigo hilo masaa machache baada ya jaribio lake la kushambulia kambi ya Jeshi la Ulinzi la Uganda (UPDF) ambalo ni sehemu ya Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (AMISOM) kutibuliwa. Wanachama kadhaa wa kundi hilo la ukufurishaji wameuawa katika operesheni hiyo.

Askari wa UPDF ambao ni sehemu ya AMISOM

Jeshi la Somalia kwa kusaidiwa na kikosi maalumu cha Umoja wa Afrika AMISOM lilifanikiwa kuwafurusha magaidi wa al Shabab katika mji mkuu Mogadishu, mwezi Agosti 2011.

Hata hivyo bado wanamgambo hao wanadhibiti maeneo ya vijijini ya kusini na katikati mwa Somalia na wanafanya mashambulizi ya mara kwa mara ya kuvizia katika mji mkuu Mogadishu na maeneo mengine.

Tags

Maoni