Sep 30, 2020 04:40 UTC
  • Sudan Kusini kufungua tena shule baada ya kupungua kesi za Covid-19

Huku nchi kadhaa za Afrika zikiendelea kulegeza sheria kali za kudhibiti maambukizi ya virusi vya Corona kutokana na kupungua kwa kasi ya maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19, serikali ya Sudan Kusini imetangaza kuwa shule nchini humo zitaanza kufunguliwa kuanzia mwezi ujao wa Oktoba.

Waziri wa Elimu wa nchi hiyo, Awut Deng Achuil amesema hatua ya kwanza ya ufunguaji wa shule itaanza Oktoba 5 na itahusisha wanafunzi 75,000 wa darasa la nane wa shule za msingi, na wanafunzi 35,000 wa kidato cha nne wa sekondari.

Achuil amesema lengo la kufunguliwa kwa shule katika kipindi cha wiki moja ijayo, ni kuwawezesha wanafunzi wakamilishe muhula wa masomo wa 2019/2020.

Waziri huyo wa Elimu wa Sudan Kusini amebainisha kuwa, wanafunzi wa shule za msingi watamaliza masomo yao mwezi Februari mwaka ujao 2021 na wale wa kidato cha nne watamaliza masomo yao mwezi Machi mwakani.

Haya yanajiri siku mbili baada ya Rwanda kupitia kwa Waziri wake wa Elimu, Valentine Uwamariya kusema shule zote zitafunguliwa ifikapo mwezi Novemba mwaka huu, na wataanza na vyuo vikuu.

Maambukizi ya virusi vya corona yamepungua kwa kiasi kikubwa 

Aidha Uganda nayo imetangaza kuwa shule za nchi hiyo hasa kwa wanafunzi wanaomaliza masomo zitafunguliwa mwezi ujao wa Oktoba kwa ajili ya mitihani ya kitaifa.

Huko nchini Kenya walimu wameanza kurejea mashuleni kama walivyoagizwa na Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) kwa ajili ya kufanya usafi na kuandaa mitaala, lakini Wizara ya Elimu inasubiriwa kutangaza tarehe ya kuanza shughuli za masomo nchini humo.

 

Tags

Maoni