Oct 02, 2020 00:41 UTC
  • Kongo, miaka 10 baada ya ripoti ya UN kuweka wazi jinai kubwa na za kutisha

Miaka 10 iliyopita, Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ilichapisha ripoti yake kuhusu utelekezaji wa haki za binadamu huko Kongo DR.

Ripoti hiyo imejumuisha vitendo vya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na sheria za kimataifa vilivyofanywa nchini humo kati ya Machi 1993 na Juni mwaka 2003.

Uchunguzi wa aina hiyo ambao haujawahi kufanywa ulikusudia kukomesha jinai hizo zilizoendelea kwa zaidi ya muongo mmoja katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.  

Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa ilieleza kuwa, wananchi wa Kongo zaidi ya milioni 4 walipoteza maisha ikiwa ni matokeo ya moja kwa moja au au yasiyo ya moja kwa moja ya mizozo iliyoikumba nchi hiyo huku mabinti na wanawake zaidi ya 40,000 wakitumiwa kama watumwa wa ngono, na watu wengine milioni tatu wakilazimika kuwa wakimbizi.

Wakimbizi wa Kongo

Licha ya kutolewa ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa, lakini hakuna jinai yoyote kati ya hizi iliyofunguliwa mashtaka; suala ambalo limelaumiwa na kukosolewa pakubwa na wananchi wa Kongo. Mmoja ya wakosoaji wa jinai hizo ni Dr. Denis Mukwege mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 2018. 

Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa imetaja vitendo 617 vya ukatili na utumiaji mabavu vilivyofanyika katika mikoa yote ya nchi hiyo na kutaja nafasi ya makundi ya Kongo na ya nchi ajinabi katika kutenda jinai hizo yakiwemo majeshi au makundi yenye silaha kutoka Rwanda, Uganda, Burundi na Angola.

Zoezi hilo la kuhakiki ukiukaji wa haki za binadamu na sheria za kimataifa nchini Kongo lililofanyika miaka kumi iliyopita kwa usaidizi wa serikali ya Kongo. Hata hivyo Shirika la Human Rights Watch limesema kuwa, mfumo wa sheria wa nchi hiyo hauna uwezo wala dhamana ya kutosha ya kuhakikisha kuwa haki inatendeka na wahusika wa jinai hizo wanachukuliwa hatua.

Vilevile watetezi wa haki za binadamu nchini Congo wamekuwa wakitishiwa kuuawa. 

Mwezi Agosti mwaka huu Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa alisema kuwa maisha ya daktari Dr. Denis Mukwege ambaye alishinda Tuzo ya Amani ya Nobel kwa kazi yake ya kutibu waathirika wa ubakaji katika vita yamo hatarini baada ya kutolewa vitisho kadhaa vya kumuua.

Maafisa wa Umoja wa Mataifa wanasema kuwa vitisho hivyo vilivyotolewa kwa Dr. Denis Mukwege na familia yake kupitia njia ya simu na mitandao ya kijamii vimehusishwa na msimamo wake wa kukosea waziwazi ukatili unaofanywa dhidi ya wanawake na ukiukaji wa haki za binadamu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. 

Mwaka 2012 pia Dr. Denis Mukwege alinusurika jaribio la mauaji.

Tags

Maoni