Oct 03, 2020 07:49 UTC
  • Duru ya pili ya mazungumzo baina ya pande hasimu Libya yaanza nchini Morocco

Duru ya pili ya mazungumzo baina ya pande hasimu nchini Libya imeanza katika katika mji wa Bouznika huko nchini Morocco ikiwa ni katika juhudi za kujaribu kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo.

Imeelezwa kuwa, lengo la mazungumzo ya mara hii pamoja na mambo mengine ni kukamilisha makubaliano yaliyofikiwa katika duru iliyotangulia ya mazungumzo hayo.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, duru ya mara hii ya mazungumzo hayo inalenga kuandaa vigezo na mikakati kwa ajili ya kuainisha viongozi ambao watachukua nyadhifa muhimu kwa mujibu wa kipengee cha 15 cha hati ya makubaliano ya Skhirat.

Hayo yaynajiri katika hali ambayo, Baraza la Uongozi la Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya linaloongozwa na Fayyez al-Sarraj limetangaza kuwa, halijatuma mwakilishi wake katika mazungumzo hayo, na kwamba, hata al-Sarraj ambaye alipatiwa mwaliko rasmi amekataa kushiriki  katika mazungumzo hayo.

 

Ijapokuwa serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya iliundwa mwaka 2015 kwa mujibu wa makubaliano na kwa usimamizi wa Umoja wa Mataifa, vikosi vitiifu kwa jenerali muasi Khalifa Haftar anayeungwa mkono na bunge la serikali ya Tabrook havikuitambua serikali hiyo; na kuanzia Aprili 4 mwaka uliopita wa 2019 vilianzisha operesheni za mashambulio kwa lengo la kuuvamia na kuukalia mji mkuu wa Libya, Tripoli.

Libya ilitumbukia katika machafuko na vita vya ndani baada ya wanajeshi wa Marekani wakishirikiana na wale wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) kuishambulia nchi hiyo na kusaidia harakati za kumuondoa madarakani aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo Kanali Muammar Gaddafi hapo mwaka 2011.

Tags