Oct 14, 2020 02:23 UTC
  • Mamia wapambana na polisi Tunisia baada ya muuza sigara kuuawa kwa buldoza

Mamia ya waandamanaji waliokuwa wakirusha mawe walipambana na polisi katika mji wa Sbeitla nchini Tunisia jana Jumanne baada ya mamlaka kushambulia kibanda cha sigara ambacho hakina leseni, na kumuua mmiliki wake aliyekuwa amelala ndani yake.

Watu walioshuhudia wamesema kuwa, wakazi wa mji maskini wa Sbeitla walifunga barabara za mji huo kwa matairi ya moto na kupambana na polisi kwa kutumia mawe.

Malmaka ya mji huo imelazimika kutumia jeshi kwa ajili ya kulinda majengo na ofisi za serikali.

Maafisa wa eneo hilo na mashuhuda wamesema muuzaji huyo wa sigara alikuwa amelala ndani ya kibanda chake wakati polisi wa manispaa walipofika na tingatinga kisha wakabamiza kibanda hicho na kumuua mmiliki wake chini ya kifusi.

Baada ya kifo cha mtu huyo kuthibitishwa na mamlaka za mji huo, Waziri Mkuu wa Tunisia, Hichem Mechichi amemfukuza gavana wa mkoa wa Kasserine, wenye mji huo wa Sheitla na maafisa watatu wa usalama wa eneo hilo katika jaribio la kupunguza hasira za wananchi.

Mji wa Sheitla uko karibu na miji inayotambuliwa kuwa maskini zaidi ya Tunisia ukiwemo wa Sidi Bouzid, ambako ndiko mapinduzi ya mwaka wa 2011 yalikoanzia baada ya muuza mboga barabarani, Mohamed Bouazizi, kujichoma moto akipinga unyanyasaji wa polisi na kunyang'anywa bidhaa zake na maafisa usalama.

Mohamed Bouazizi

Mapinduzi hayo yaliiondoa madarakani serikali ya dikteta wa zamani wa Tunisia, Zine El Abidine Ben Ali na kuchochea mapinduzi yaliyoziondoa madarakani tawala kadhaa katika nchi za Kiarabu.

Tags