Oct 16, 2020 02:39 UTC
  • Sudan yakanusha kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni

Duru moja ya kuaminika ndani ya Baraza la Uongozi la Sudan imekanusha taarifa zinazodai kuwa kumefikiwa makubaliano ya kuanzishwa uhusiano wa kawaida baina ya baraza hilo na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Jumatano usiku, mtandao wa Kizayuni wa i24 ulidai kuwa, Baraza la Uongozi la Sudan hatimaye limekubaliana na pendekezo la Marekani la kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel baada ya majadiliano ya wiki moja. Mtandao huo umedai kuwa makubaliano hayo yamefikiwa katika kikao kilichofanyika Jumatano usiku.

Hata hivyo afisa huo mwandamizi wa Baraza la Uongozi la Sudan, jana Alkhamisi alikanusha habari hiyo na kusema kwamba siku ya Jumatano baraza hilo halikufanya kikao chochote kile.

Siku ya Jumatano, vyombo vya habari vya Sudan na vya ulimwengu wa Kiarabu vilitangaza kwamba Marekani imeipa Sudan makataa ya masaa 24 kuhakikisha kuwa inakubali kuwa na uhusiano wa kawaida na Israel ili jina la Sudan litolewe katika orodha ya Washington ya eti waungaji mkono ugaidi.

 

Kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa Sudan imekuwa ikifanya juhudi za kuhakikisha jina lake linatolewa katika orodha ya Marekani ya eti nchi zinazounga mkono ugaidi wa kiserikali. Kuweko jina la Sudan katika orodha hiyo kulikodumu kwa miaka 30 sasa kumekata mawasiliano ya kifedha baina ya Sudan na benki za kimataifa.

Katika mazungumzo yaliyofanyika wiki iliyopita katika mji mkuu wa Imarati, Abu Dhabi, baina ya Marekani na Sudan, wajumbe wa Marekani walidai kwamba kama Sudan itatangaza uhusiano wa kawaida na Israel basi itaondolewa kwenye orodha hiyo.

Wananchi, vyama vya siasa na makundi mbalimbali ya Sudan yamelionya vikali Baraza la Uongozi la nchi hiyo, lisithubutu kutangaza uhusiano wa kawaida na Wazayuni.

Tags