Oct 18, 2020 14:13 UTC
  • Mpwa wa Rais wa Tanzania atishia 'kummaliza' Tundu Lissu kwa sindano ya sumu

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi CCM nchini Tanzania ametishia kumuua kwa kumdunga sindano ya sumu, mgombea urais wa nchi hiyo kwa tiketi cha Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Tundu Lissu kwa kile alichosema kuendelea 'kuwajaza upepo' wafuasi wake ili waandamane.

Kheri James, ambaye pia ni mpwa wa Rais John Pombe Magufuli anayegombea tena urais kwa tiketi ya chama tawala CCM ameonekana akitoa kitisho hicho katika mkanda wa video uliosambaa leo kwenye mitandao ya kijamii akiwa katika mkutano wa kampeni za chama chake kuelekea uchaguzi mkuu wa Tanzania utakaofanyika Oktoba 28. 

James, ambaye ni mwenyekiti taifa wa UVCCM ametoa kitisho cha kuua, baada ya Lissu, ambaye ndiye mgombea anayechuana vikali na Magufuli katika uchaguzi huo kusisitiza kuwa, endapo itafanyika mizengwe na uchakachuaji katika zoezi zima la uchaguzi ikiwemo kutomtangaza mshindi halisi wa uchaguzi wa rais, atahamasisha wafuasi wake waandamane nchi nzima kudai haki yao.

Kheri James (aliyevaa magwanda wa kijani) na Tundu Lissu (aliyevalia magwanada ya kaki)

Kauli ya mwenyekiti huyo wa UVCCM ya kutumia neno 'safari hii' na kueleza kwamba watatumia kile kilichofahamika katika maelezo yake kama sindano ya sumu ili kumuua Tundu Lissu imetilia nguvu tuhuma kuwa 'watu wasiojulikana' waliompiga risasi 16 Lissu katika shambulio la Septemba mwaka 2017 wana na uhusiano na vyombo vya usalama vya dola au chama tawala CCM.

Hii si mara ya kwanza kwa mpwa huyo wa Rais wa Tanzania kutoa kauli nzito za kutishia uhai wa watu hasa wapinzani. Itakumbukwa kuwa, akiwa ni kiongozi wa chama aliwahi kutamka kwamba, mtu yeyote aliyechoka kuishi, ajaribu kufanya vurugu siku ya uchaguzi. Hata hivyo Kheri James, ambaye ni kiongozi mwandamizi wa CCM hakufuatiliwa na vyombo vya usalama vya dola wala kuwajibishwa na chama chake tawala kwa kauli yake hiyo.

Katika kampeni zake, Tundu Lissu, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema, ambacho ni chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, amekuwa akikosoa vikali utendaji wa serikali ya awamu ya tano ya Tanzania hasa Rais John Magufuli mwenyewe, akimtuhumu pamoja na mambo mengine kwamba, miaka mitano ya uongozi wake imeshuhudia kukithiri kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa katika serikali zote zilizopita mauaji, utekaji nyara raia unaofanywa na watu wasiojulikana na kuwekwa magerezani kwa miaka kadhaa bila kushtakiwa Waislamu wengi wakiwemo mashekhe kwa tuhuma bandia za ugaidi.../

 

Tags