Oct 20, 2020 03:14 UTC
  • Nasruddin Abdul Bari
    Nasruddin Abdul Bari

Serikali ya Sudan imetangaza kuwa inajadiliana na Mahakama ya Kimataiifa ya Jinai (ICC) mapendekezo matatu kuhusu jinsi ya kumfungulia mashtaka rais wa zamani wa nchi hiyo, Omar al Bashir, na wenzake kadhaa kwa tuhuma za kutenda jinai dhidi ya binadamu na jinai za kivita katika jimbo la Darfur.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Sheria wa Sudan, Nasruddin Abdul Bari, baada ya mazungumzo yake na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya ICC, Fatou Bensouda mjini Khartoum. Abdul Bari amesisitiza kuwa Sudan iko tayari kushirikiana na mahakama hiyo kwa mujibu wa sheria za kimataifa zinazoshughulikia wahalifu.

Ameongeza kuwa Sudan imetoa mapendekezo matatu kuhusu kesi ya al Bashir na wenzake ambayo ni ama kuanzishwa mahakama maalumu, kufunguliwa mahakama mseto inayoshirikisha serikali ya Khartoum na ICC, au kupelekwa watuhumiwa hao katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai huko The Hague nchini Uholanzi.

Al Bashir anakabiliwa na tuhuma za kutenda jinai dhidi ya binadamu huko Darfur

Waziri wa Sheria wa Sudan amesema kuwa pande hizo mbili bado zinajadili mapendekezo hayo.

Kwa upande wake Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, Bi Fatou Bensouda amepongeza mazungumzo ya ujumbe wa mahakama hiyo na serikali ya Sudan bila ya kutoa maelezo zaidi.

Bensouda anajaribu kuwashawishi viongozi wa Sudan waafiki suala la kukabidhiwa al Bashir na maafisa wengine kadhaa wa zamani wa nchi hiyo ili wahukumiwe katika mahakama ya kimataifa ya ICC.

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) inamtuhumu Omar al Bashir kwamba alihusika na mauaji ya kimbari dhidi ya wakazi wa eneo la Darfur huko magharibi mwa Sudan na vilevile kutenda jinai dhidi ya binadamu na imetoa kibali cha kutiwa nguvuni mtuhumiwa huyo.

Tags

Maoni