Oct 20, 2020 07:39 UTC
  • Sudan yakubali kuipa Marekani dola milioni 335 iondolewe katika orodha ya ugaidi

Rais Donald Trump amesema Marekani itaiondoa Sudan katika orodha ya nchi 'zinazounga mkono ugaidi' baada ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika kukubali kuipa Washington dola milioni 335.

Katika ujumbe wake wa Twitter uliojaa dharau na majigambo, Trump amesema hatimaye Sudan imekubali kutoa dola milioni 335 kama fidia kwa familia za wahanga wa mashambulizi ya kundi la al-Qaida nchini humo.

Trump ameandika katika ujumbe huo kuwa: Habari Njema! Serikali mpya ya Sudan, ambayo inapiga hatua, imekubali kuilipa Marekani dola milioni 335, kama fidia kwa familia za wahanga wa ugaidi. Mara tu fedha hizo zitakapotumbukizwa (katika hazina ya Marekani), nitaiondoa Sudan katika orodha ya Madola yanayounga mkono ugaidi.

Duru zilizo karibu na serikali ya mpito ya Sudan zimedokeza kuwa, Khartoum ipo tayari kuipa Marekani fidia hiyo ikiwa na hamu ya kuondolewa vikwazo vilivyolemaza uchumi wa nchi hiyo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa US, Mike Pompeo (Kushoto) alipoenda Sudan kuishawishi ianzishe uhusiano na Israel

Itakumbukwa kuwa mwaka 1993 wakati wa utawala wa Omar al-Bashir, Marekani iliiweka Sudan katika orodha ya nchi zinaounga mkono ugaidi na matokeo yake ni kwamba, Sudan ilizuiwa misaada ya kifedha na mikopo ya Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia.

Wadadisi wa mambo wanasema kuwa, baada ya Khartoum kukubali kuburuzwa na Marekani kulipa fidia hiyo, haitakuwa na budi kukubali shinikizo jingine la Washington la kuitaka ijiunge na mkumbo wa baadhi ya nchi za Kiarabu wa kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Israel.

Tags

Maoni