Oct 21, 2020 12:54 UTC
  • Sheria ya kutotoka nje Nigeria yatangazwa baada ya ghasia na kuuawa waandamanaji

Sheria ya kutotoka nje imetangazwa katika mji wa Lagos nchini Nigeria huku ghasia zikienea nchini humo kupinga ukatili wa polisi.

Taarifa zinasema watu kadhaa walifariki hapo jana mjini Lagos, Nigeria, baada ya wanajeshi kuwafyatulia risasi za moto waandamanaji wanaopinga ukatili wa polisi. Shirika la kimataifa la Amnesty limesema, limepata habari za kuaminika kuwa watu 20 waliuawa jana katika ghasia mjini Lagos.

Kufuatia ghasia hizo amri ya kutotoka nje ndani ya saa 24 imewekwa mjini Lagos na miji mingine na hivyo kuwalazimisha mamilioni ya watu kutotoka nje.

Lagos ni moja ya majimbo matatu kati ya 36 ya Nigeria yaliyotangaza hatua kama hiyo katika siku mbili zilizopita. Mkuu wa polisi wa kitaifa pia aliamuru kupelekwa mara moja kwa vikosi vya kupambana na ghasia kote nchini kufuatia kuongezeka kwa mashambulio kwenye vituo vya polisi, kulingana na msemaji wa polisi.

Maandamano ya kupinga ukatili wa polisi Nigeria

Rais Muhammadu Buhari Jumanne alifanya mazungumzo na Waziri wa Ulinzi na Mkuu wa vikosi vya ulinzi kujadili usalama wa kitaifa, kulingana na maafisa wawili kutoka ofisi ya rais, wakizungumza na shirika la habari la Reuters kwa sharti la kutotajwa majina.

Msemaji wa rais hakupatikana kutoa maoni yake juu ya madai hayo ya utumiaji wa risasi dhidi ya waandamanaji.

Kwa zaidi ya wiki mbili, maelfu ya raia wa Nigeria wamekuwa wakiandamana kote nchini humo dhidi ya ukatili unaofanywa na Kikosi Maalum cha Kupambana na Ujambazi (SARS).

Maandamano hayo yalizuka baada ya video kuanza kusambaa mitandaoni mwanzoni mwa mwezi huu inayowaonyesha maafisa wa SARS wakimpiga risasi mtu mmoja kusini mwa jimbo la Delta. Polisi walikana kuhusika na tukio hilo la kutumia risasi.

Tags

Maoni