Oct 21, 2020 12:58 UTC
  • Waangalizi wa AU, ECOWAS waridhia uchaguzi wa Guinea, Conde aongoza

Waangalizi wa Umoja wa Afrika (AU) na Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika Magharibi (ECOWAS) wamepongeza uchaguzi wa Jumapili katika Jamhuri ya Guinea na kusema kuwa, ulikuwa huru na wa haki.

Kauli hiyo ya Jumanne imetolewa siku moja baada ya mpinzani mkuu Celloud Dalein Diallo kudai kuwa alishinda katika uchaguzi huo na hivyo kuandaa uwanja wa makabiliano na Rais Alpha Conde. Tangazo hilo la Diallo limepingwa vikali na tume ya  uchaguzi.

Tayari Rais  Conde ametangazwa kushinda majimbo manne hadi sasa huku kura zikiendelea kuhesabiwa nchini humo, kufuatia uchaguzi wa rais wa Oktoba 18. Matokeo hayo ya awali yametangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Guinea. Hadi sasa Conde amepata kura nyingi zaidi katika majimbo matatu ya mji mkuu, Conakry.

 

Tume ya uchaguzi ya Guinea inatazamiwa kutangaza matokeo ya awali baada ya siku tatu. Mahakama ya Katiba itakuwa na siku nane kutangaza mshindi.

Uchaguzi huo umefanyika wakati kumekuwa na maandamano dhidi ya serikali ambayo yamepelekea makumi ya watu kupoteza maisha.

Uchaguzi huo wa rais ulikuwa na wagombea 12 lakini mahasimu wakuu ni rais wa sasa Alpha Conde, mwenye umri wa miaka 82 na Cellou Dalein Diallo, kiongozi wa chama cha upinzani cha Union of Democratic Forces of Guinea (UFDG).

Wagombea wanahitajika kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura zote ili kutangazwa mshindi, au vinginevyo kutalazimika kuwa na duru ya pili ambayo itafanyika Novemba 24 ya mwezi ujao.

Maoni