Oct 21, 2020 13:00 UTC
  • Burundi yaadhimisha miaka 27 tangu kutokea mauaji ya Melchior Ndadaye

Burundi leo Jumatano tarehe 21 Oktoba imefanya kumbukumbu ya miaka 27 tangu kuuawa Rais Melchior Ndadaye, kiongozi wa kwanza aliyechaguliwa nchini humo chini ya misingi ya kidemokrasia.

Melchior Ndadaye rais wa kwanza, kutoka jamii ya Wahutu, aliyechaguliwa katika misingi ya kidemokrasia aliauawa usiku wa Oktoba 21 mwaka 1993 na kundi la wanajeshi kutoka jamii ya Watutsi wenye msimamo mkali ambao walishindwa kuvumilia kuona mtu kutoka jamii ya Wahutu akiongoza nchi hiyo, iliyotawaliwa na Watutsi kwa miaka zadi ya 31.

Melchior Ndadaye aliibuka mshindi kwenye uchaguzi wa mwezi Julai mwaka 1993 dhidi ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo,Pierre Buyoya chini ya chama chake cha SAHWANYA -FRODEBU. Ndadaye hakupata muda wa kuongoza nchi hiyo kwani miezi mitatu tu baadaye aliuawa, na hivyo kuzuka machafuko ya kikabila nchini humo, yaliosababisha maelfu kwa maelfu ya watu.

Rais wa zamani wa Burundi Pierre Buyoya, ambaye kwa sasa ni Mwakilishi wa Umoja wa Afrika nchini Mali ni miongoni mwa waliohukumiwa kifungo cha maisha jela

 

Hayo yanajiri katika hali ambayo Jumatatu iliyopita Mahakama Kuu ya Burundi ilitoa uamuzi wake katika kesi ya wale wanaotuhumiwa kuhusika na kushiriki katika mauaji ya rais wa kwanza wa nchi hiyo Melchior Ndadaye.

Rais wa zamani wa Burundi Pierre Buyoya, ambaye kwa sasa ni Mwakilishi wa Umoja wa Afrika nchini Mali, pamoja na viongozi wengine 18 waandamizi, raia na wanajeshi wa jeshi la zamani, wakati huo likitawaliwa na kabila la walio wachache la Watutsi, wamehukumiwa kifungo cha maisha hasa kwa "shambulizi dhidi ya rais wa nchi ". Viongozi wengine watatu wamehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa kosa la kushiriki katika mauaji hayo. Mtu mmoja tu wa wakati huo amefutiwa mashitaka. 

Maoni