Oct 22, 2020 02:38 UTC
  • Tanzania yapatiwa mkopo wa mamilioni ya dola kwa ajili ya kukabiliana na Corona

Benki ya Maendeleo Afrika imeidhinisha mkopo wa dola milioni 50.7 kugharamia kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19 nchini Tanzania.

Taarifa zinaeleza kuwa, mkopo huo utasaidia mpango wa serikali ya Tanzania wa dola milioni 109 za Marekani sawa na bilioni 252 za Tanzaniawa  kupambana na virusi vya corona unaogharamiwa kwa pamoja na serikali na wadau wengine wa maendeleo katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Mpango huo unalenga kuimarisha uchumi kwa kupunguza athari za janga hilo katika jamii na kiafya hasa biashara za wenyeji, walio katika hatari ya kuathirika na mfumo wa afya.

Tanzania kama nchi zingine imekuwa ikipambana kuhakikisha uchumi wake hauathiriki kwa kiasi kikubwa na janga hilo huku Benki ya Dunia ikithibitisha kwamba nchi hiyo imeingia kwenye pato la kati.

Hata hivyo mkopo huo unaidhinishwa katika hali ambayo, Rais John Pombe Magufuli alitangaza Julai mwaka huu kwamba, Tanzania haina tena virusi vya Corona.

Rais John Pombe Magufuli

 

Tanzania iliacha kutangaza takwimu za idadi ya maambukizi ya virusi hivyo mwezi Aprili mwaka huu, baada ya maafisa wa maabara ya taifa kutuhumiwa kutoa matokeo yasiyo sahihi.

Mapema mwezi Mei mwaka huu Shirika la Afya Duniani (WHO) lilikanusha madai ya Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli kwamba vipimo vya virusi vya Corona vina hitilafu.

Kuna wengi wanaojiuliza kuhusiana na ukweli wa kauli ya serikali ya Tanzania ya kufanikiwa kukabiliana na virusi vya Corona hasa kutokana na kutotangazwa takwimu kama yanavyofanya mataifa mengine ya dunia.