Oct 23, 2020 03:01 UTC
  • Afisa wa Sudan: Nchi inakaribia kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni

Afisa mmoja wa Sudan ambaye hakutaka jina lake litajwe amedai kuwa muda wa nchi hiyo kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel umekaribia licha ya vyama mbalimbali na wananchi kupinga jambo hilo.

Baada ya kutangazwa habari ya ziara ya ujumbe wa Marekani na utawala wa Kizayuni nchini Sudan na ujumbe huo kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo; kiongozi wa ngazi ya juu wa Sudan jana Alhamisi alisema kuwa ndege iliyotua juzi Jumatano katika uwanja wa ndege wa Khartoum ilikuwa imewabeba maafisa wa Israel na Marekani. 

Katika mazungumzo hayo ya Khartoum, ujumbe wa Kizayuni na Marekani ulichunguza hatua zinazohusiana na kuliondoa jina la Sudan katika orodha ya nchi zinazounga mkono ugaidi, na suala la kuanzisha uhusiano kati ya Khartoum na Tel Aviv. 

Duru za habari za Kizayuni pia zimeripoti kuwa, Sudan imekubali kuanzisha uhusiano kamili na Tel Aviv. 

Weledi wa mambo wanasema kuwa, mchakato wa kuanzisha uhusiano baina ya tawala za nchi za Kiarabu na Tel Aviv unafungamana pakubwa na maslahi ya kisiasa ya Rais Donald Trump wa Marekani na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni; kwa sababu kila mmoja alihitaji ujanja wa kidiplomasia kutokana na matatizo ya kisiasa yanayowakabili.  

Kwa msingi huo ni serikali ya Trump ndiyo inayoshinikiza pakubwa na kuibana serikali ya Sudan ili itangaze haraka kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni. 

Wananchi wa  Sudan wapinga nchi yao kuanzisha uhusiano na Israel 

 

Tags

Maoni