Oct 24, 2020 07:41 UTC
  • Raia 51, maafisa usalama 18 wameuawa katika maandamano ya ghasia Nigeria

Makumi ya watu wameuawa katika machafuko na maandamano yanayoendelea kushuhudiwa katika maeneo mbalimbali ya Nigeria.

Katika taarifa iliyotolewa usiku wa kuamkia leo, Ofisi ya Rais Muhammadu Buhari imesema kwa akali raia 51 na maafisa usalama 18 wamepoteza maisha katika ghasia na makabiliano baina ya raia na maafisa usalama.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, raia wengine 37 wamejeruhiwa katika maandamano hayo ya fujo ambayo serikali inadai kuwa yamechochewa na magenge ya majambazi yaliyotoka nyara maandamano ya amani ya wananchi.

Akihutubia taifa juzi Alkhamisi, Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria aliwahimiza vijana kusitisha maandamano na kushirikiana na serikali kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa matatizo yaliyopo.

Maandamano ya kulaani ukatili wa polisi Nigeria

Hata hivyo amekosolewa vikali ndani na nje ya nchi kwa kutoashiria kadhia ya maafisa usalama kuwapiga risasi na kuua makumi ya raia waliokuwa wakiandamana katika hotuba yake hiyo.

Amri ya kutotoka nje imetangazwa katika majimbo kadhaa ya nchi hiyo ili kudhibiti maandamano na machafuko yanayoendelea nchini humo kwa zaidi ya wiki mbili sasa. Raia wa Nigeria wamekuwa wakiandamana kote nchini humo wakipinga ukatili unaofanywa na Kikosi Maalum cha Kupambana na Ujambazi (SARS).

Tags

Maoni