Oct 25, 2020 02:37 UTC
  • Kuanzishwa uhusiano baina ya Sudan na utawala haramu wa Israel na mustakbali wa nchi hiyo

Hatimaye Sudan imesalimu amri mbele ya mashinikizo ya Marekani na kukubali kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Israel. Sambambana na kutangaza habari hiyo, Rais Donald Trump wa Marekani amesema kuwa, amewasilisha uamuzi wake wa kuliondoa jina la Sudan katika orodha ya nchi zinazounga mkono ugaidi kwenye Kongresi ya nchi hiyo.

Mwaka 1993 na baada ya kushambuliwa jengo la Kituo cha Biashara cha Kimataifa mjini New York, Marekani ililiweka jina la Sudan katika orodha yake ya nchi zinazounga mkono na kufadhili ugaidi. Katika miaka ya mwishoni mwa uongozi wake, rais wa zamani wa Sudan, Omar al Bashir alifanya jitihada kubwa za kuona jina la nchi hiyo linaondolewa katika orodha hiyo kwa kubadili siasa za serikali ya Khartoum na hata kufuata sera na matakwa ya Marekani na waitifaki wake. Baada ya matukio ya mwaka jana yaliyopeleka kuondolewa madarakani al Bashir, serikali ya mpito ya nchi hiyo ililipa kipaumbele suala la kuondoa jina la Sudan katika orodha ya magaidi ya Marekani. Katika miezi kadhaa iliyopita maafisa wa serikali ya Sudan walifanya mazungumzo mara kadhaa na maafisa wa Marekani ambayo imefanya jihihada za kufaidika na hali hiyo na nafasi dhaifu ya Sudan; hivyo walitilia maanani suala la kuishinikiza Khartoum ili ianzishe uhusiano na utawala haramu wa Israel sambamba na kadiri uchaguzi wa rais wa Marekani ulivyokuwa ukikaribia. 

Rais aliyepinduliwa wa Sudan, Omar al Bashir  

Katika miezi miwili iliyopita nchi za Bahrain na Imarati zimesaini makubaliano ya kuanzisha uhusiano na utawala ghasibu wa Israel chini ya upatanishi wa Marekani. Sudan inakuwa nchi ya tatu kujiunga na mkumbo huo chini ya mradi huo khabithi wa maafisa wa serikali ya Washingon. Matatizo makubwa ya kiuchumi, uhaba wa chakula, ukosefu wa ajira na umaskini, hitilafu za ndani na vita vinavyoendelea katika baadhi ya maeneo ya Sudan, na vilevile maambukizi ya virusi vya corona  na uhaba wa dawa na vifaa vya tiba, yote kwa pamoja yameifanya nchi hiyo itumbukie katika mgogoro mkubwa. Hali hii imetumiwa na maafisa wa Washington na Tel Aviv kwa ajili ya kuiburuta Sudan katika meza ya mazungumzo na kuitwisha matakwa yao. Vilevile suala la kuondoa jina la Sudan katika orodha ya Marekani ya waungaji mkono wa ugaidi na kupata misaada ya kifedha na kiuchumi ya Washington vimetumiwa kama chambo cha kuwashawishi maafisa wa Khartoum kwa ajili ya kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Israel.  

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Abdel Bari Atwan anasema: Sudan ina historia na turathi kubwa katika medani ya kupambana na utawala haramu wa Israel na kuunga mkono Umma wa Kiislamu. Lengo kuu ni kuharibu historia na turathi hiyo. Lengo ni kuvunjilia mbali na kuharibu mapinduzi na harakati za Sudan za kupigania uhuru, haki za binadamu na ustawi wa kiuchumi. Inaonekana kuwa, kumeanza jitihada za kupora matunda ya mapinduzi ya wananchi wa Sudan na kuyatumia katika malengo mengine."
Habari ya kuanzishwa uhusiano wa kidiplomasia baina ya Sudan na utawala haramu wa Israel imepokewa kwa masikitiko makubwa na vyama na wananchi wa Sudan. Vyama vingi vya siasa vikiwemo vya Kongresi ya Taifa na al Baath vimetoa taarifa tofauti vikipinga uamuzi wa utawala wa nchi hiyo wa kuanisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel na kutangaza kuwa, vitaunda kambi ya kitaifa ya kupinga suala hilo.
Kiongozi wa chama cha Umma, Sadiq al Mahdi amewatahadharisha watawala wa kijeshi na serikali ya mpito ya nchi hiyo kuhusu matokeo mabaya ya hatua ya kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Israel na kusema chama cha Umma kitabatilisha uungaji mkono wake kwa serikali ya mpito. 
Inatabiriwa kuwa siku sijazo Sudan itakuwa katika hali ngumu na huenda ikatumbukia katika mgogoro mkubwa.  

Sadiq al Mahdi, kiongozi wa chama cha Umma nchini Sudan 

  

Tags