Oct 25, 2020 08:20 UTC
  • Watoto wasiopungua 6 wauawa katika shambulio la  waasi nchini Cameroon

Watoto wasiopungua 6 wameuawa katika shambulio la watu wenye silaha lililolenga shule ya Fransisca International Bi-lingual Academy. Shambulio hilo lilifanyika jana katika eneo la Koumba kusini magharibi mwa Cameroon.

Picha za video zimeonyesha miili ya watoto hao wanafunzi waliouawa ikiwa imejaa damu sakafuni. Mwanafunzi  aliyeshuhudia kwa macho uvamizi huo ameeleza kuwa, alisikia milio ya risasi na kukimbia kujificha. Ameongeza kuwa, walikuwa darasani wakifundishwa lugha ya kifaransa wakati aliposikia milio ya risasi. Amesema mwalimu wao alikuwa mtu wa kwanza kukimbia. 

Itakumbukwa kuwa, shule katika maeneo ya Cameroon yanayozungumza Kiingereza zilifunguliwa wiki mbili zilizipita baada ya kusimamishwa masomo kufuatia machafuko ya makundi ya wanamgambo na kutokana na maambukizi ya virusi vya corona.

Serikali ilitoa ahadi ya kuzilinda taasisi za elimu nchini humo baada ya kushuhudiwa vitendo mbalimbali vya uhalifu dhidi ya raia. Kundi la waasi la Ambazonia linalopigania kujitenga na kuwa huru maeneo ya kaskazini na kusini mwa Cameroon limetuhumiwa kufanya mauaji ya jana huko Cameroon. 

Tags