Oct 25, 2020 12:10 UTC
  • Dina Mufti
    Dina Mufti

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Ethiopia ameyataja matamshi yaliyotolewa na Rais Donald Trump wa Marekani kuhusu bwawa la Renaissance kuwa ni jinai na uhalifu.

Dina Mufti alikuwa akijibu matamshi ya Donald Trump aliyesema kuwa, kuna uwezekano Misri ikaliripua bwawa hilo linalojengwa na Ethiopia juu ya maji ya Mto Nile.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ethiopia amesema kuwa, nchi yake ina haki ya kutumia maliasili zake kwa ajili ya maendeleo ya watu wa Ethiopia.

Dina Mufti amesisitiza kiwa, hakuna nchi yenye haki ya kuitwisha Ethiopia maoni na matakwa yake na kwamba dola lolote lile duniani haliwezi kusitisha mradi wa ujenzi wa bwawa la Renaissance.

Wakati huo huo balozi wa zamani wa Mrekani nchini Ethiopia amesema kuwa Washington imejitoa katika nafasi ya patanishi katika mgogoro wa ujenzi wa bwawa la Renaissance baada ya matamshi yaliyotolewa na Donald Trump. 

Donald Trump

David Chen amesema hii si mara ya kwanza kwa Marekani kuchukua msimamo wa upendeleo kwa maslahi ya Misri. Balozi huyo wa zamani wa Marekani nchini Ethiopia ameeleza kushangazwa na matamshi ya Donald Trump kuhusu bwawa la Renaissance akisema Washington imekuwa mchochezi katika mgogoro huo badala ya kuzishajiisha pande mbili kufikia mapatano. 

Katika matamshi yake ya kwanza aliyotoa kuhusu kadhia ya bwawa la Renaissance lililojengwa na Ethiopia na ambalo limezusha mvutano, Rais Donald Trump wa Marekani alisema juzi kuwa, kuna uwezekano Misri ikaliripua bwawa hilo.

Misri na Sudan zinasema ujenzi wa bwawa hilo ambalo limegharimu karibu dola bilioni nne, utapunguza maji ya nchi hizo na hivyo kuvuruga maisha ya mamilioni ya watu. Ethiopia nayo inasisitiza kuwa ujenzi wa bwawa hilo ni muhimu kwa ajili ya kueneza umeme katika nchi hiyo ili kuimarisha sekta ya viwanda na pia kuuza bidhaa hiyo katika nchi za nje.

Tags

Maoni