Oct 26, 2020 11:40 UTC
  • Wahamiaji 11 akiwemo mjamzito wafa maji Libya wakielekea Ulaya

Wahajiri 11 akiwemo mwanamke mjamzito wamefariki dunia katika Bahari ya Mediterania baada ya boti yao kuzama, huko pwani ya Libya.

Safa Msehli, Msemaji wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) amesema ajali hiyo ilitokea jana Jumapili, na kwamba hiyo ni ajali ya tatu kuripotiwa katika pwani ya Libya ndani ya wiki moja.

Amesema wavuvi na wapigambizi wa Gadi ya Pwani ya Libya wamefanikiwa kuwanusuru wahamiaji 10 katika ajali hiyo, na kuwarejesha ufukweni.

Jumanne iliyopita, watu wasiopungua 15 walikufa maji katika Bahari ya Mediterania baada ya boti yao kuzama, huko huko pwani ya Libya.

Ajali za kuzama boti za wajahiri wa Kifrika zimekuwa zikiripoti mara kwa mara

Takwimu za Shirika la Kimataifa la Uhamiaji zinaonyesha kuwa, wahajiri zaidi ya 500 aghalabu yao wakiwa ni raia wa Afrika wamepoteza maisha katika ajali hizo za majini, wakiwa na azma ya kuelekea Ulaya kusaka maisha mazuri.

Mgogoro mkubwa wa wahajiri unaozizonga nchi za Ulaya umesababishwa na sera mbaya za nchi za Magharibi katika maeneo mbalimbali ya dunia hususan Asia Magharibi na vilevile umaskini mkubwa na ukosefu wa usalama katika baadhi ya nchi za Afrika.    

Tags

Maoni