Oct 26, 2020 11:50 UTC
  • Kiongozi wa upinzani Ushelisheli ashinda urais baada ya kujaribu mara 6

Mgombea wa upinzani katika uchaguzi wa rais huko katika kisiwa cha Ushelisheli ameibuka mshindi baada ya kupata asilimia 54.9 ya kura zilizopigwa.

Wavel Ramkalawan ameibuka mshindi katika uchaguzi huo uliofanyika juzi Jumamosi, na kumbwaga rais anayeondoka Danny Faure aliyepata asilimia 43 ya kura.

Danny Lucas, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Ushelisheli jana Jumapili alimtangaza Ramkalawan kuwa mshindi halali wa uchaguzi wa urais kisiwani humo.

Takriban watu 74,000 waliotimiza masharti ya kupiga kura walishiriki zoezi hilo la kidemokrasia la kumchagua rais na wabunge katika kisiwa hicho kilichoko katika Bahari ya Hindi mashariki mwa Afrika, na chenye jamii ya watu karibu 97 elfu.

Wananchi wa Ushelisheli wakipiga kura

Akilihutubia taifa baada ya kutangazwa mshindi, Ramkalawan amesema, "Mimi na Faure (rais anayeondoka) ni marafiki wakubwa. Uchaguzi haumaanishi mwisho wa kuchangia mazuri kwa taifa lake. Katika uchaguzi huu, hakuna mshindi na aliyeshindwa, taifa zima limepewa fursa ya kuibuka mshindi." 

Hii ni mara ya sita kwa kinara huyo wa upinzani wa chama cha Seychelles Democratic Alliance kugombea kiti cha rais. Mwaka 2015, alishindwa kwa kura 193 na James Michel katika duru ya pili ya uchaguzi wa rais.

 

Tags

Maoni