Oct 27, 2020 07:50 UTC
  • Al Burhan: Bunge la Sudan linaweza kubadilisha uamuzi kuhusu makubaliano tuliyofikia na Israel

Kiongozi wa baraza la utawala la Sudan ametetea makubaliano ya kuaibisha iliyofikia serikali ya mpito ya nchi hiyo na Israel na kudai kuwa bunge la Sudan linaweza kuupitia upya uamuzi huo wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni.

Jenerali Abdel Fattah al Burhani amedai pia kwamba, katika mchakato wa mashauriano asilimia 90 ya makundi ya kisiasa nchini Sudan hayakuonyesha upinzani wowote kwa mpango wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel.

Kiongozi huyo wa baraza la utawala la Sudan ametoa madai hayo wakati vyama vingi vya siasa vya nchi hiyo si tu vimetangaza kuwa vinapinga uamuzi wa serikali ya mpito wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni lakini vimesisitiza pia kwamba vina nia ya kuanzisha kambi ya kitaifa ya kupinga mapatano hayo.

Hivi karibuni, Baraza la Fiqhi la Sudan lilieleza katika taarifa kwamba, ni haramu kuanzisha uhusiano wa aina yoyote na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Abdel Fattah al Burhan na Benjamin Netanyahu

Ijumaa ya tarehe 23 Oktoba Rais Donald Trump wa Marekani alitangaza kuwa Sudan na Israel zimefikia mapatano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida wa kidiplomasia, ikiwa na maana ya Sudan kujiunga na nchi zingine za Kiarabu na Kiislamu za Misri, Jordan, Imarati na Bahrain kuutambua rasmi utawala huo haramu wa Kizayuni unaoikalia kwa mabavu Palestina na Quds tukufu.

Nchi kadhaa za Kiarabu zimeamua kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel ilhali kwa miaka na miaka sasa utawala huo wa Kizayuni umekuwa ukiendeleza jinai na ukandamizaji dhidi ya wananchi madhulumu wa na kuyakalia kwa mabavu maeneo mengi ya ardihi za nchi za Kiislamu na Kiarabu.../

Tags

Maoni