Oct 27, 2020 08:20 UTC
  • Watu kadhaa waripotiwa kuuawa na kujeruhiwa Pemba, Tanzania katika ghasia za kabla ya upigaji kura ya mapema

Watu kadhaa wanaoaminika kuwa wafuasi wa chama cha ACT Wazalendo wameripotiwa kuwa wameuawa na kujeruhiwa usiku wa kuamkia leo kisiwani Pemba, Zanzibar kabla ya kufanyika upigaji kura ya mapema ambao umezusha taharuki visiwani humo.

Taarifa rasmi iliyotolewa mapema leo na Mwenyekiti wa chama hicho Seif Sharif Hamad imedai kuwa watu watatu ambao wametambuliwa kuwa ni Asha Haji Hassan, Yussuf Shaame Muhidin na Kombo Hamad Salum wameuawa kwa kupigwa risasi na askari polisi usiku wa kuamkia leo huko katika kijiji cha Kangagani kilichoko kwenye jimbo la Ole kisiwani Pemba katika vurumai za kuwatawanya wananchi waliokuwa wakijaribu kuzuia mpango wa kupelekwa kwenye vituo vya kupigia kura masanduku yanayodaiwa kuwa na kura ambazo zilikuwa tayari zimeshapigwa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya chama cha ACT, watu wengine tisa wamejeruhiwa katika vurumai hizo. Imeelezwa kuwa, awali askari polisi walijaribu kutumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya bila mafanikio watu hao na ndipo walipotumia risasi hai na kusababisha vifo vya watu hao watatu na kujeruhiwa wengine tisa.

Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Seif Sharif Hamad

Hadi sasa hakuna maelezo yaliyotolewa na jeshi la Polisi kuthibitisha au kukanusha taarifa hiyo ya ACT.

Wasiwasi na mivutano ya kisiasa imetanda visiwani Zanzibar tangu Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ZEC ilipotangaza utaratibu mpya wa upigaji kura wa siku mbili za tarehe 27 na 28 Oktoba ili kuruhusu watendaji wa tume hiyo na askari wa vikosi vya ulinzi wanaosimamia zoezla uchaguzi kupiga kura ya mapema leo, kabla ya zoezi rasmi la upigaji kura lililopangwa kufanyika kesho la kumchagua rais wa Zanzibar, wawakilishi na madiwani.

Chama kikuu cha upinzani visiwani humo cha ACT Wazalendo kimekuwa kikidai kuwa, utaratibu huo mpya unalenga kufanya uchakachuaji wa kura kwa maslahi ya chama tawala CCM, dai ambalo limekanushwa na ZEC.

Mbali na Zanzibar, kesho Jumatano uchaguzi mkuu wa rais wa Tanzania, wabunge na madiwani utafanyika nchini kote ambapo mchuano mkali katika uchaguzi wa Tanzania ni kati ya Rais John Magufuli anayewania kwa tiketi ya CCM na Tundu Lissu, mgombea wa chama kikuu cha upinzani nchini humo Chadema.

Wagombea wakuu katika uchaguzi wa rais wa Zanzibar ni Dkt  Hussein Mwinyi wa CCM na Maalim Seif Sharif Hamad wa ACT Wazalendo.../ 

 

Tags