Oct 27, 2020 11:34 UTC
  • Umoja wa Afrika wataka Nigeria ichukue hatua za kusitisha ghasia, mauaji

Umoja wa Afrika umeihimiza serikali ya Nigeria ichukue mara moja hatua za amani za mazungumzo ili kupunguza mvutano unaozidi kupamba moto nchini humo, kufanya uchunguzi kuhusu mauaji na kuwafikisha wahusika mahakamani.

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Afrika anayeshughulikia mambo ya wanawake, amani na usalama Bi. Bineta Diop, ametuma salamu za rambi rambi kwa familia za waliouawa katika ghasia za karibuni nchini Nigeria.

Aidha ameahidi kuunga mkono juhudi za Nigeria na kufanya ushirikiano na shirika la Mtandao wa Viongozi wa Wanawake wa Afrika nchini Nigeria (AWLN) na kuongeza mchango wa wanawake katika kutafuta suluhisho la kudumu, ili kuhakikisha amani na usalama wa watu wa Nigeria.

Makumi ya watu wameuawa katika machafuko na maandamano yanayoendelea kushuhudiwa katika maeneo mbalimbali ya Nigeria.

Katika taarifa iliyotolewa Ijumaa, Ofisi ya Rais Muhammadu Buhari imesema kwa akali raia 51 na maafisa usalama 18 wamepoteza maisha katika ghasia na makabiliano baina ya raia na maafisa usalama.

Maandamano ya kupinga ukatili wa polisi Nigeria

Amri ya kutotoka nje imetangazwa katika majimbo kadhaa ya nchi hiyo ili kudhibiti maandamano na machafuko yanayoendelea nchini humo kwa zaidi ya wiki mbili sasa. Raia wa Nigeria wamekuwa wakiandamana kote nchini humo wakipinga ukatili unaofanywa na Kikosi Maalum cha Kupambana na Ujambazi (SARS).

Serikali ya Nigeria imekosolewa vikali ndani na nje ya nchi kutokana na ukatili ambao umekuwa ukitekelezwa na maafisa wa usalama nchini humo dhidi ya raia wanaoandamana kwa amani.

Tags

Maoni