Oct 27, 2020 12:54 UTC
  • Mwito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuelekea uchaguzi mkuu wa Tanzania

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), António Guterres ametaka mchakato mzima wa uchaguzi nchini Tanzania kuwa huru na haki.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, Guterres amewataka viongozi wote wa kisiasa na wafuasi wao kushiriki zoezi hilo la kidemokrasia la hapo kesho kwa amani na kujiepusha na vurugu.

Kauli ya Katibu Mkuu wa UN imekuja katika hali ambayo, watu kadhaa wanaoaminika kuwa wafuasi wa chama cha ACT Wazalendo wameripotiwa kuwa wameuawa na kujeruhiwa usiku wa kuamkia leo kisiwani Pemba, Zanzibar kabla ya kufanyika upigaji kura ya mapema ambao umezusha taharuki visiwani humo.

Katika hatua nyingine, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania, Simon Sirro ametoa wito kwa Watanzania katika kipindi hiki cha uchaguzi kujihadhari na mihemko isiyokuwa na tija inayoweza kuwaletea matatizo. Akizungumza nawaandishi wa habari hii leo, IGP Sirro amesema kila mtu anategemewa na familia yake, hivyo ni vyema kuepuka vurugu zinazoweka kuharibu amani iliyopo.

Amesema, “Kama unajua hutopiga kura usiwe sehemu ya kuanzisha vurugu kwakuwa hapo jana usiku huko Pemba kipindi tunasambaza masanduku ya kupigia kura Polisi walirushiwa mawe hivyo hatutarajii kitendo hicho kujirudia.”

Watanzania wa Bara na visiwani kuelekea katika masanduku ya kupigia kura kesho Jumatano

Amesema kuna maisha baada ya uchaguzi na kwamba ushindani wowote lazima mmoja ashindena hata kama aliyeshinda ni adui yako unatakiwa uvumilia.

Mbali na Zanzibar, kesho Jumatano uchaguzi mkuu wa rais wa Tanzania, wabunge na madiwani utafanyika nchini kote ambapo mchuano mkali katika uchaguzi wa Tanzania ni kati ya Rais John Magufuli anayewania kwa tiketi ya CCM na Tundu Lissu, mgombea wa chama kikuu cha upinzani nchini humo Chadema.

Wagombea wakuu katika uchaguzi wa rais wa Zanzibar ni Dkt  Hussein Mwinyi wa CCM na Maalim Seif Sharif Hamad wa ACT Wazalendo.

Tags