Oct 28, 2020 04:47 UTC
  • Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania  (kulia) na kiongzi wa chama cha upinzani Chadema Tundu Lissu
    Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania (kulia) na kiongzi wa chama cha upinzani Chadema Tundu Lissu

Mamilioni ya raia wa Tanzania leo wanaelekea katika masanduku ya kupiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani.

Upigaji kura unaanza baada ya kampeni kali za miezi miwili ambapo wagombea wa vyama mbali mbali walinadi sera zao ili kuwavutia wapiga kura.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Tanzania (NEC) Jaji Semistocles Kaijage, kuna wapiga kura milioni 29.188 ambao wamejiandikisha katika Daftari la Kudumu la NEC na wengine 566.352 wameandikishwa katika Daftari la Kudumu la Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

Aidha alisema kuna junla ya vituo vya kupiga kura 81.567 vituo 80,155 vilivyo na daftarli la NEC na vituo 1,412 vya ZEC. Kwa ujumla vyama 15 vinasimamisha wagombea urais huku ushindani mkali ukionekana kati ya mgombea wa urais kwa tikiti ya chama tawala CCM Dkt. John Pombe Magufuli, ambaye anatabiriwa kushinda na Tundu Lissu wa chama kikuu cha upinzani CHADEMA.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa  António Guterres ametaka mchakato mzima wa uchaguzi nchini Tanzania kuwa huru na haki.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari, Guterres amewataka viongozi wote wa kisiasa na wafuasi wao kushiriki zoezi hilo la kidemokrasia la leo kwa amani na kujiepusha na vurugu.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania IGP Simon Sirro

Kauli ya Katibu Mkuu wa UN imekuja katika hali ambayo, watu kadhaa wameripotiwa kuuawa katika ghasia ambazo zimeibuka kisiwani Pemba, Zanzibar kabla ya kufanyika upigaji kura ya mapema jana. Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na chama cha upinzani cha ACT Wazalendo watu hao waliuawa katika kisiwa cha Pemba kwa kupigwa risasi. Hata hivyo,akizungumza na vyombo vya habari jijini Dar es Salaam Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania IGP Simon Sirro amekanusha kutokea mauaji na badala yake amesema jeshi hilo limewakamata vijana 42 kutokana na ghasia zilizoshuhudiwa Pemba hapo jana. Sirro pia alitoa onyo kwa watu binafsi na makundi ya watu wanaopanga kusalia katika vituo vya kupigia kura baada ya kupiga kura akisema hilo halitakubalika. IGP Sirro amesema kwamba shughuli ya kulinda kura itafanywa na mawakala wa vyama husika. Aidha amewataka raia kutoshawishiwa au kujiingiza katika vurugu za aina yoyote zitakazozua vurugu. Upigaji kura umeanza saa moja asubuhi na utaendelea hadi saa 10 jioni.

 

Tags

Maoni