Oct 28, 2020 07:48 UTC
  • Imarati yaipa Sudan mamilioni ya dola baada ya kuanzisha uhusiano na Israel

Umoja wa Falme za Kiarabu umeipa Sudan msaada wa dola nusu bilioni za Marekani, siku chache baada ya Khartoum kukubali kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Shirika rasmi la habari la Imarati la WAM limetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi (ADFD)  umeipa Sudan dola milioni 556.5 kama msaada wa kifedha, ili kuunusuru uchumi, sekta za afya, elimu, chakula na kilimo za nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Mohammed Saif Al Suwaidi, Mkurugenzi Mkuu wa ADFD amedai kuwa, msaada huo ni sehemu ya ruzuku ya dola bilioni 1.5 ya Imarati kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya msingi ya wananchi wa Sudan.

Wiki iliyopita, Marekani ilitangaza habari ya kufikiwa mapatano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida baina ya Sudan na Israel. Washington ilidai kuwa makubaliano hayo yanalenga kuanzishwa uhusiano wa kiuchumi na kibiashara baina ya Sudan na utawala dhalimu wa Israel.

Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani alipoitembelea Sudan

Khartoum ilichukua hatua hiyo muda mfupi baada ya Rais Donald Trump kusema kuwa Marekani itaiondoa Sudan katika orodha ya nchi 'zinazounga mkono ugaidi' baada ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika kukubali kuipa Washington fidia ya dola milioni 335.

Itakumbukwa kuwa mwaka 1993 wakati wa utawala wa Omar al-Bashir, Marekani iliiweka Sudan katika orodha ya nchi zinaounga mkono ugaidi, jambo lililopelekea Sudan inyimwe misaada ya kifedha na mikopo ya Mfuko wa Fedha wa Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia.

Tags