Oct 28, 2020 07:55 UTC
  • Majeshi ya Jubaland na Kenya yatibua shambulio la al-Shabaab Somalia

Askari wa Kikosi Maalumu cha Jubaland wakishirikiana na askari wa Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) wamefanikiwa kuzima shambulizi la kigaidi la kundi la wanamgambo wa al-Shabaab katika eneo la Lower Jubba, kusini mwa Somalia.

Duru za kiusalama zimeripoti kuwa, wanachama wa kundi hilo la kigaidi na kitakfiri walikabiliwa vikali na wanajeshi wa Somalia na Kenya usiku wa kuamkia jana na hatimaye wakatimuliwa.

Inaarifiwa kuwa, magaidi hao walivamia kambi ya jeshi ya KDF katika mji wa Tabta ulioko katika eneo la Lower Jubba katika jimbo lenye mamlaka ya ndani la Jubalanda, lakini wakalazimika kutoroka baada ya kukabiliwa vikali kwa risasi.

Katika hatua nyingine, wapiganaji wanne wa kundi hilo la kigaidi wameuawa katika mapambano makali yaliyotokea kwenye mji wa Qansah Dhere katika mkoa wa kusini wa Bay.

Mkuu wa mji wa Qansah Dhere, Abdi Ibrahim alisema hayo jana na kuongeza kuwa, wapiganaji hao waliangamizwa baada ya kushambulia msafara wa magari uliokuwa umebeba wanajeshi wa serikali ukielekea katika kambi ya jeshi la serikali katika mji huo.

Wanajeshi wa KDF ya Kenya wakikabiliana na magaidi Somalia

Amebainisha kuwa, walifanikiwa kuwaua wapiganaji wanne wa kundi hilo katika makabiliano hayo ya Jumapili, na kwamba mwanajeshi mmoja wa serikali pia aliuawa.

Tangu mwaka 2007, kundi la kigaidi la al-Shabaab lenye mfungamano na mtandao wa al Qaida limekuwa likifanya mashambulizi ndani ya Somalia kwa lengo la kuiangusha serikali kuu ya nchi hiyo inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.

Tags