Oct 28, 2020 10:48 UTC
  • Uchaguzi Mkuu Tanzania; kilele cha vuta nikuvute baina ya chama tawala na upinzani

Wananchi wa Tanzania waliotimiza masharti ya kupiga kura leo wameelekea katika masanduku ya kupiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa rais, wabunge na madiwani na hivyo kutumia haki yao ya kikatiba.

Zoezi la kupiga kura limefanyika leo baada ya kampeni kali za uchaguzi za miezi miwili zilizogubikwa na changamoto na matukio mengi. Tume ya Uchaguzi ya Tanzania imetangaza kuwa, jumla ya wapiga kura milioni 29.188 wamejiandikisha katika Daftari la Kudumu la NEC na wengine 566.352 wameandikishwa katika Daftari la Kudumu la Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC). Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi, vituo vya kupiga kura 81.567 vituo 80,155 vilivyo na daftarli la NEC na vituo 1,412 vya ZEC viliandaliwa kwa ajili ya uchaguzi wa leo. Vyama 15 vya kisiasa vimesimamisha wagombea urais huku ushindani mkali ukionekana kati ya mgombea wa urais kwa tiketi ya chama tawala CCM Dkt. John Pombe Magufuli, ambaye anatabiriwa kushinda na Tundu Lissu wa chama kikuu cha upinzani CHADEMA ambaye anatarajiwa kutoa ushindani mkali na ambaye katika miaka ya hivi karibuni amekuwa mwiba kwa serikali ya Magufuli.

Uchunguzi wa maoni wa hivi karibuni ulionyesha kuwa, Rais John Pombe Magufuli ambaye anawania kutetea kipindi chake cha pili cha miaka mitano ataibuka na ushindi mkubwa katika uchaguzi wa leo.

Rais Magufuli akipiga kura leo Chamwino Dodoma

 

Chama cha Rais John Pombe Magufuli CCM kimetawala Tanzania tangu nchi hiyo ilipopata uhuru mwaka 1961 kutoka kwa mkoloni Muingereza. Magufuli aliingia madarakani mwaka 2015 akiahidi kukomesha ubadhirifu na ufisadi na kuboresha miundombinu pamoja na mambo mengine. Hata hivyo mfumo wake mgumu wa utawala umepelekea kupewa jina la Bulldozer; jina ambalo awali alipewa wakati akiwa waziri.

Licha ya kupongezwa kwa hatua mbalimbali za maendeleo zilizochukuliwa na serikali yake, zikiwemo za kustawisha miundomsingi ya kiuchumi na kupambana na ufisadi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anakosolewa kuwa anaminya na kukandamiza demokrasia sambamba na kuendesha kampeni ya kuua vyama vya upinzani katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki. Hata hivyo, serikali ya Magufuli inakanusha vikali madai hayo ikisisitiza kuwa, wapinzani hawapaswi kukiuka sheria kwa kisingizio cha demokrasia na uhuuru wa kufanya mikutano.

Pamoja na hayo wanasiasa wa upinzani wanasisitiza kuwa serikali ya Rais Magufuli iliweka mazingira magumu ya kufanya mikutano ya kisiasa na kukandamiza demokrasia. 

Maalim Seif Sharif Hamad, mgombea urais Zanzibar kwa tiketi ya ACT-Wazalendo akipiga kura yake

 

Aidha vyama vya upinzani vinalalamikia kile vinachokitaja kuwa, kuandamwa viongozi wao na kesi mbalimbali, hali ambayo inawafanya washindwe kufanya shughuli za kuimarisha vyama vyao kwani kila mara wapo mahakamani au magereza.

Katika upande mwingine, makundi ya kutetea haki za binadamu yanamtuhumu Rais Magufuli kwamba alizidisha vitendo vya ukandamizaji katika kipindi cha kuelekea katika uchaguzi sambamba na kutoa vitisho kwa wapinzani wa kisiasa na kwa vyombo vya habari, tuhuma ambazo zilikanushwa na serikali yake.

Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, kuna mambo kadhaa ambayo yanakipa kila sababu chama tawala cha Mapinduzi CCM kushinda uchaguzi wa leo na pengine chaguzi nyingine zijazo. Mosi, kushindwa wapinzani kuungana na kusimamisha mgombea mmoja mwenye nguvu atakayeweza kukabiliana na mgombea wa chama tawala. Pili, nafasi kubwa iliyojijengea CCM hasa katika maeneo ya vijijini. Tatu, maendeleo makubwa aliyoyafanya Rais Magufuli katika miaka yake mitano ya awali na jinsi alivyofanikiwa kupambana na ufisadi, licha ya kuweko malalamiko ya hapa na pale ya wananchi ya kupungua mzunguko wa pesa. Nukta ya nne ambayo ndio kilio cha siku zote cha wapinzani ni kutofanyika mabadiliko ya katiba na kuweko tume huru ambayo itafanya shughuli zake na kuakisi kwa maana halisi mfumo wa vyama vingi nchini humo.

Wapiga kura nchini Tanzania wakiwa katika foleni wakisubitri kupiga kura 

 

Visiwani Zanzibar pia ambayo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano upinzani mara hii unatarajiwa kushuhudiwa kati ya chama cha CCM na kile cha ACT-Wazalendo. Mwanasiasa mkongwe Maalim Seif Sharif Hamad baada ya kuhamia chama cha upinzani cha ACT, mara hii anawania urais kwa tiketi ya chama hicho akichuana na Hussein Mwinyi wa CCM.

Uchaguzi visiwani humo unafanyika baada ya kuripotiwa vitendo vya mauaji hapo jana, ingawa polisi kupitia Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Tanzania IGP Simon Sirro imekanusha taarifa za kutokea mauaji na badala yake imesema jeshi hilo limewakamata vijana 42 kutokana na ghasia zilizoshuhudiwa huko Pemba.

Ala kulli haal, kile kinachoonekana wazi ni kuwa, uchaguzi wa leo nchini Tanzania ni kilele cha vuta nikuvute baina ya chama tawala na mrengo wa upinzani; uchaguzi ambao unaweza kuchora ramani ya njia na kuainisha mustakabali wa upinzani katika uga wa siasa za nchi hiyo.

Maoni