Oct 28, 2020 12:23 UTC
  • Maandamano ya kupinga uhusiano na utawala wa Kizayuni yanaendelea nchini Sudan

Maandamano ya wananchi wa Sudan ya kupinga uamuzi wa serikali ya nchi hiyo wa kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel yanaendelea.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Anadolu, wananchi wa Sudan leo wameendelea na maandamano yao mbele ya jengo la Waziri Mkuu wa nchi hiyo mjini Khartoum na kukiita kitendo cha serikali ya mpito ya nchi hiyo cha kutangaza uhusiano wa kawaida na Wazayuni kuwa ni usaliti kwa Uislamu na Waislamu.

Ripoti hiyo imeongeza kuwa, waandamanaji wamebeba mabango yenye maandishi mbalimbali kama yanayosema: "Quds ni mali yetu" na "Mapatano na Wazayuni ni usaliti."

Majenerali wa kijeshi nchini Sudan wameingia kwenye mkumbo wa kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala katili wa Kizayuni baada ya nchi nyingine mbili za Kiarabu za Imarati na Bahrain kutangulia kuingia kwenye mkumbo huo.

Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) inafanya juu chini kuziburuza nchi nyingine za Kiarabu kwenye mkumbo huo ikiwemo hongo. 

Viongozi wa Imarati na Sudan ambao wako mstari wa mbele kuchochea uhusiano wa kawaida na Wazayuni

 

Mfano wa jambo hilo ni taarifa zinazosema kuwa, Imarati imeipa hongo Sudan kwa jina la msaada wa dola nusu bilioni za Marekani, siku chache baada ya Khartoum kukubali kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Shirika rasmi la habari la Imarati la WAM limetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi (ADFD)  umeipa Sudan dola milioni 556.5 kama msaada wa kifedha, ili kunusuru uchumi wake na kuboresha sekta za afya, elimu, chakula na kilimo za nchi hiyo.

Tags

Maoni