Oct 28, 2020 12:27 UTC
  • Watanzania washiriki kwa wingi katika upigaji kura leo

Mamilioni ya Watanzania, leo Jumatano, Oktoba 28, 2020 wamejitokeza katika vituo vya kupigia kura kwa ajili ya kuwachagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar, wabunge wa Bunge la Muungano, madiwani na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.

Uchaguzi huo umefanyika leo kote nchini Tanzania huku kukiwa na taarifa za kuuawa na kujeruhiwa watu kadhaa kisiwani Pemba, usiku wa kuamkia jana Jumanne. 

Mchuano mkali katika uchaguzi wa marais upo baina ya Maalim Seif Sharif Hamad wa chama cha ACT Wazalendo na Dk Hussein Ali Hassan Mwinyi  wa chama tawala wa CCM kwa upande wa serikali ya Zanzibar, na baina ya Tundu Lissu wa Chama cha Maendeleo ya Demokrasia (CHADEMA) na Rais John Pombe Magufuli wa chama tawala wa CCM katika uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hadi tunaanzaa habari hii kulikuwa kumeripotiwa matukio tofauti kama vile kutiwa mbaroni na kuachiliwa mgombea wa Ubunge wa chama cha Chadema, Halima Mdee katika jimbo la Kawe jijini Dar es Salaam. 

Wapiga kura wakishiriki katika uchaguzi mkuu nchini Tanzania. Jumatano, Oktoba 28, 2020

 

Rais Magufuli ameshiriki katika upigaji kura huo akiwa pamoja na mkewe Jijini Dodoma. Akizungumza baada ya kupiga kura katika kituo cha Chamwino, Rais Magufuli amesema: “Napenda niwapongeze wasimamizi wa uchaguzi hapa Chamwino; maandalizi yalikuwa mazuri na watu wamejitokeza kwa wingi, wito wangu kwa Watanzania tujitokeze kwa wingi kupiga kura pia nipende kusisitiza amani.”

Kwa upande wa Zanzibar, mgombea urais Zanzibar kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Hussein Mwinyi, amepiga kura Mjini Unguja na ametoa mwito kwa Wazanzibari kuendelea kujitokeza vituoni kwa ajili ya kupiga kura.

Naye mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama cha ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif, amepiga kura katika kituo cha Garagara, Jimbo la Mwera mapema leo Jumatano, Oktoba 28, 2020 na kusema, ametiwa moyo na kujitokeza watu wengi katika vituo vya kupigia kura ila amegundua wananchi wengi wana malalamiko ya kutokuona majina yao kwenye vituo walivyojiandikisha.

Katika upande mwingine, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania (NEC), Dk Wilson Mahera mapema leo asubuhi alisema kuwa, kuanzia leo usiku Jumatano Oktoba 28, 2020 tume hiyo itaanza kupokea matokeo ya kura za urais kutoka kwenye majimbo.

Tags