Oct 29, 2020 08:21 UTC
  • Freeman Mbowe
    Freeman Mbowe

Matokeo ya awali ya uchaguzi wa Bunge nchini Tanzania yanaonyesha kuwepo mpambano mkali kati ya chama tawala CCM na chama kikuu cha upinzani Chadema; ambapo upinzani umeonekana kupoteza viti vingi.

Mwenyekiti Taifa wa Chadema amekuwa kiongozi na mbunge wa zamani wa kwanza wa chama hicho kushindwa kutetea nafasi yake ya ubunge baada ya mshindani wake kutangazwa kuwa mshindi jimbo la Hai. Freeman Mbowe ambaye amepata kura 27 elfu amebwagwa na Saasisha Mafuwe wa CCM aliyepata kura 89,786.

Aidha mgombea ubunge kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt Tulia Ackson ametangazwa kuwa mshindi wa nafasi ya ubunge katika jimbo la Mbeya Mjini. Dkt Tulia Akson alimshinda mpinzani wake wa karibu kutoka chama cha Chadema Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu kwa kujipatia kura 75,225. Sugu amepata kura 37, 591.

Jimbo la Moshi Mjini ambalo limekuwa chini ya upinzani tangu uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi 1995, safari hii mgombea wa CCM, Priscus Tarimo ameitoa CCM kimasomaso kwa kushinda uchaguzi huo. Kadhalika Madiwani wa CCM wameshinda kata zote 20 katika jimbo la Arumeru Mashariki.

Wagombea wakuu wa urais Tanzania Bara na Zanzibar

Huku hayo yakiarifiwa, mgombea wa chama cha CUF, Shamsia Mtamba ameshinda ubunge wa jimbo la Mtwara vijijini baada ya kupata kura 26,262, dhidi ya mpinzani wake Hawa Ghasia wa CCM aliyepata kura 18,505. Shamsia alikuwa mbunge wa viti maalumu kupitia chama cha CUF kabla ya kuamua kuwania ubunge jimbo la Mtwara vijijini.

Matokeo mengine yaonyesha kuwa, CCM imetwaa ubunge na viti vyote vya udiwani katika jimbo la Shinyanga.

Mamilioni ya Watanzania, jana Jumatano walijitokeza katika vituo vya kupigia kura kwa ajili ya kuwachagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar, wabunge, wawakilishi na madiwani. 

Tags

Maoni