Oct 29, 2020 12:17 UTC
  • Askari wa MONUSCO kuhamishia shughuli zao mashariki mwa DRC

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Tume ya Umoja wa Mataifa ya kusimamia amani nchini humo, MONUSCO, wamewasilisha hati kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa inayopangilia kuondolewa kwa walinda amani na kuvunja kambi zote za kikosi hicho.

Mikoa ya kwanza inayohusika ni Kasaï ya Kati na Kasaï ambapo kambi za kikosi cha MONUSCO katika mikoa hiyo zinatarajiwa kufungwa ifikapo mwaka 2021. Taarifa zaidi zinasema kuwa kwa mara nyingine tena, Umoja wa Mataifa unataka kurudi kwenye mikoa mikuu mitatu mashariki mwa nchi hiyo ambayo imekuwa ikisumbuliwa na ukosefu wa amani.

Eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo  limekuwa likishuhudia machafuko ya mara kwa mara baina ya makundi ya wanamgambo kwa upande mmoja na wanamgambo na maafisa usalama kwa upande mwingine, kutokana na kuwa na utajiri mkubwa wa madini hususan dhahabu na almasi. 

Waasi wa ADF

 

Mashirika mbalimbali ya utoaji misaada ya kibinadamu yamekuwa yakionya kuhusiana na hali mbaya ya kibinadamu katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo na kutoa wito wa kukomeshwa machafuko.

Wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongohasa wa mashariki mwa nchi hiyo wamekuwa wakilalamikia utendaji mbovu wa askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa MONUSCO na hata kuandamana wakitaka kuondoka askari hao katika nchi yao.

Harakati za makundi ya waasi mashariki mwa nchi hiyo kama za ADF-Nalu la Uganda zimevuruga kabisa usalama katika maeneo hayo na kusababisha raia wengi kulazimika kuyakimbia makazi yao.