Oct 29, 2020 12:20 UTC
  • Kura zaendelea kuhesabiwa Tanzania; Lissu atangaza kupinga matokeo

Zoezi la kuhesabu kura linaendelea nchini Tanzania kufuatia Uchaguzi Mkuu uliofanyika jana ambao upinzani unadai ulikumbwa na udanganyifu, madai ambayo yamekanushwa vikali na tume ya uchaguzi ya nchi hiyo.

Matokeo ya uchaguzi huo yanaendelea kutolewa hatua kwa hatua na tayari yanaonyesha kuwa, wapinzani wamepata pigo kubwa katika majimbo muhimu ya Ubunge.

Wabunge muhimu wa upinzani wamesindwa kutetea nafasi zao za Ubunge baada ya chama tawala CCM kutwaa majimbo hayo. 

Aidha matokeo ya awali ya urais na udiwani yanaonyesha kuwa chama tawala cha CCM kimepata ushindi mkubwa. Visiwani Zanzibar pia matokeo ya awali yanaonyesha kuwa, mgombea wa CCM Hussein Mwinyi anaongoza akiamuacha nyuma mwanasiasa mkongwe Maalif Seif Sharif Hamad wa ACT-Wazalendo.

Upinzani unadai kuwa, waangalizi wake walifukuzwa katika baadhi ya vituo vya kupigia kura. Kwa upande mwengine chama cha upinzani ACT-Wazalendo kimesema, mawakala wake walishuhudia kupokonywa kwa masanduku ya kura na vyombo vya usalama, kujaza kura za ziada kwenye masanduku na wapiga kura kufukuzwa na maafisa waliosema karatasi za kura zilikuwa zimeisha.

Tundu Lissu mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA akiongea na waandishi wa habari

 

Kwa upande wake Tume ya Kitaifa ya Uchaguzi, NEC, imesema madai hayo si kweli na  hayana msingi wowote. Wakati huo huo, raia wa Tanzania bado wanalalamikia ukosefu wa mitandao ya kijamii jambo ambalo limefanya iwe changamoto kwao kuwasiliana na wengine au kuwasilisha maoni kwenye majukwaa mbalimbali.

Wakati huo huo, mgombea wa urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, ametangaza kutokubali matokeo ya uchaguzi yanayoendelea kutangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). 

Amedai kuwa kuwa uchaguzi huo ulianza kuingia dosari mapema katika kuapisha mawakala ambao ndiyo waangalizi wa uchaguzi kwa niaba ya chama chao.

Aidha amewataka Watanzania kudai haki yao kwa njia ya demokrasia na siyo kwa vurugu yoyote huku akisema jumuiya za kimataifa pamoja na jumuiya za kikanda ziingilie kati taarifa za matokeo ya uchaguzi wa Tanzania.

 

Maoni