Oct 29, 2020 22:55 UTC
  • Hussein Mwinyi
    Hussein Mwinyi

Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imemtangaza Dr. Hussein Mwinyi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwa Rais Mteule wa Zanzibar baada ya kupata ushindi wa kura 380,402 sawa na 76.27%. akifuatiwa na Maalim Seif Sharif Hamad wa chama cha ACT Wazalendo aliyepata kura 96,103 sawa na asilimia 19.87.

Akitangaza matokeo hayo jana Mwenyekiti wa ZEC, Jaji Hamid Mahamoud Hamid alisema kuwa, wagombea urais walikuwa 17 na waliopiga kura 498,786 sawa na asilimia 88.07 ya wapiga kura 566,352 waliojiandikisha.
Jaji Hamid amesema kura zilizoharibika zilikuwa 10,944 sawa na asilimia 2.19.  

Baada ya kutangazwa mshindi Dr. Hussein Mwinyi alisema amepokea ushindi kwa mikono miwili na kwamba anashukuru kuwa wananchi waliowengi wamemchagua yeye na chama chake Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa miaka 5 ijayo.

"Nawashukuru kwa uvumilivu na ustahamilivu mkubwa. Niwashukuru zaidi kwa kunipigia kura za kutosheleza kuwa Rais wa Zanzibar. Nitalipa imani hii kwa utumishi uliotukuka," amesema Dr. Mwinyi.

Hussein Mwinyi aliongeza kusema kuwa Zanzibar mpya itajengwa na Wazanzibari wote bila kujali itikadi zao na kwamba, Zanzibar ni kubwa na muhimu kuliko tofuati za Wazanzibari.

Amesema ushindi huo ni wa Wazanzibari wote na kusisitiza kuwa uchaguzi sasa umekwisha na umewadia wakati wa kujenga Zanzibar mpya".

Mwinyi amewahimiza wafuasi wa CCM washerehekee kwa staha bila ya kukwaza wengine kwa kuwa ushindi wasingepata pasipo kuwa na ushindani.

Kwa upande wa uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, matokeo ya awali yanaonyesha kuwa John Pombe Magufuli wa chama tawala cha CCM alikuwa akiongoza kwa kura nyingi akimuacha mbali mpinzani wake wa karibu, Tundu Lissu anayekiwakilisha chama cha CHADEMA. 

Chama tawala cha CCM pia kinaongoza katika matokeo ya uchaguzi wa Bunge kwa mujibu wa matokeo ya majimbo yaliyotangazwa hadi usiku wa kuamkia leo. 
Katika Upande mwingine aliyekuwa mgombea urais Zanzibar kwa tiketi ya  ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad pamoja na mgombea mwenza Profesa Omar Fakih wameachiwa huru kwa dhamana.

Maalim Seif Sharif Hamad

Wawili hao ambao waliachiwa huru jana usiku wametakiwa kuripoti kituo cha polisi mapema leo asubuhi. 
Maalim Seif alikamatwa jana mchana wakati alipokuwa akijiandaa kwenda eneo la Mzunguko wa Michenzani kwa ajili ya maandamano, muda mfupi baada ya kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa uchaguzi akisema hakuridhishwa na mchakato wake.

Tags

Maoni