Oct 31, 2020 11:59 UTC
  • Waivory Coast wanachagua rais leo, hali inatajwa kuwa tete

Mamilioni ya wananchi wa Ivory Coast wameelekea kwenye masanduku ya kupigia kura hii leo Jumamosi katika uchaguzi wa rais huku kukiwepo wasiwasi wa kutokea ghasia na machafuko makubwa baada ya kambi ya upinzani kutoa wito wa kususiwa uchaguzi huo.

Wapinzani wa Ivory Coast wamesusia uchaguzi huo wakipinga hatua ya Rais wa sasa wa nchi hiyo, Alassane Ouattara ya kugombea tena kwa mara ya tatu mfululizo.

Watu wasiopungua 30 wameuawa katika ghasia za kabla ya uchaguzi, suala lililoibua kumbukumbu ya machafuko ya mwaka 2010-11 ambayo yalipelekea kuuliwa watu 3,000.
Rais wa zamani wa Ivory Cost, Henri Konan Bedie na vilevile Waziri Mkuu wa zamani Pascal Affi N'Guessan wanatajwa kuwa wapinzani wakubwa zaidi wa Ouattara katika uchaguzi wa leo.

Viongozi wa upinzani wametoa wito wa kususiwa uchaguzi na kufanyika uasi wa kiraia, ingawa hawajaondoa rasmi majina ya wagombeaji wao.

Wapinzani wanapinga muhula wa tatu wa Alassane Ouattara

Ouattara, mwenye umri wa miaka 78, alitakiwa kung'atuka madarakani baada ya kipindi chake cha pili madarakani na kutoa nafasi kwa kizazi kipya, lakini inaonekana kuwa kifo cha ghafla cha aliyetayarishwa kuwa mrithi wake kililazimisha mabadiliko katika kambi ya chama tawala. 

Mwaka 2016 Katiba ya Ivory Coast ya ilibana kipindi cha mtu kugombea urais. Kwa mujibu wa marekebisho hayo ya katiba, mtu yeyote haruhusiwi kugombea urais kwa zaidi ya mihula miwili ya miaka mitano mitano.

Hata hivyo wafuasi wa Rais Alassane Ouattara wanasema kuwa, marekebisho ya Katiba ya mwaka 2016 yalifuta yote yaliyopita kabla ya hapo kwa maana kwamba Ouattara anahesabiwa kana kwamba hajawahi kugombea urais hata mara moja. 

Madai hayo yanapingwa na kambi ya upinzani na baadhi ya wanasheria ambao wanasema kuwa, kugombea tena urais Alassane Ouattara ni kinyume cha sheria. 

Tags