Oct 31, 2020 13:13 UTC
  • Chadema na ACT Wazalendo vyapinga matokeo ya uchaguzi mkuu Tanzania, Waangalizi wasema ulifuata taratibu

Vyama vya upinzani nchini Tanzania vya CHADEMA na ACT Wazalendo vimesema kuwa havitambui matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28 yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

Katika mkutano wao wa pamoja uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam, vyama hiyo vimetoa tamko lenye matakwa kadhaa ambayo ni kufanyika uchaguzi wa marudio pamoja na kuundwa Tume Huru itakayosimamia uchaguzi huo wa marudio.

Vyama hivyo pia vimelaani vurugu zilizoibuka maeneo mbalimbali nchini Tanzania kipindi chote cha uchaguzi.

Tamko la vyama hivyo limetolewa masaa kadhaa baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kumtangaza mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), John Pombe Magufuli kuwa ndiye mshindi wa kinyang'anyiro hicho.  

Magufuli aliibuka mshindi baada ya kupata ushindi wa kura 12,516,252 sawa na asilimia 84.4 ya kura zote halali zilizopigwa.

Kwa upande wa urais wa Zanzibar, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) imemtangaza Dr. Hussein Mwinyi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwa Rais Mteule wa Zanzibar baada ya kupata ushindi wa kura 380,402 sawa na 76.27%. akifuatiwa na Maalim Seif Sharif Hamad wa chama cha ACT Wazalendo aliyepata kura 96,103 sawa na asilimia 19.87.

Hussein Mwinyi ametangazwa mshindi wa uchaguzi wa rais Zanzibar

Waangalizi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamesema kuwa, uchaguzi Mkuu wa Tanzania umefanyika kwa kufuata taratibu. 

Rais Mstaafu wa Burundi, Sylvestre Ntibantunganya ambaye ndiye kiongozi wa wajumbe 89 waliosambazwa Tanzania kufuatilia uchaguzi huo, amesema kuwa, kumekuwep hali ya usalama katika maeneo mbalimbali na kwamba watu walifanya kampeni kwa uhuru kabla ya kuanza shughuli ya upigaji kura. 

Kiongozi huyo amesema kuwa, timu yake imekutana na wadau mbalimbali wa uchaguzi wakiwemo wa vyama vya siasa na waangalizi wengine. 

Timu ya waangalizi hao wa Afrika Mashariki imetoa wito kwa vyama vya siasa kufuata taratibu za kisheria kwa ajili ya kuonyesha kutoridhishwa kwao na matokeo ya uchaguzi. Vilevile imevitaka vyama vya siasa kuweka mbele maslahi ya Watanzania ikiwa ni pamoja na amani na kuepuka vitendo vyovyote vya uvunjivu wa amani. 

Tags

Maoni