Nov 01, 2020 03:27 UTC
  • Rais Magufuli wa Tanzania aendelea kupongezwa kimataifa baada ya ushindi katika uchaguzi

Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania anaendelea kupongezwa kimataifa kutokana na ushindi mkubwa alioupata katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 28.

Pongezi hizo zimekuja  baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kumtangaza mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), John Pombe Magufuli kuwa ndiye mshindi wa kinyang'anyiro hicho. 

Magufuli aliibuka mshindi baada ya kupata kura 12,516,252 sawa na asilimia 84.4 ya kura zote halali zilizopigwa.

Tundu Lissu kutoka chama cha upinzani cha Chadema ameshika nafasi ya pili kwa kupata kura 1,933,271 ya kura zote zilizopigwa.

Jumla ya watu 15,91950 walipiga kura wakati waliojiandikisha kupiga kura walikuwa 29,754,699 kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Marais wa nchi jirani za Kenya, Uganda na Burundi walikuwa miongoni mwa viongozi wa kwanza kumpongeza Magufuli kutokana na ushindi huo.

Katika ujumbe wake wa pongezi, Rais Evariste Ndayishimiye amesema, kwa niaba yake na watu wa Burundi anampongeza Magufuli kwa ushindi.

Naye Rais Yoweri Museveni wa Uganda katika ujumbe aliotuma kupitia ukurasa wake wa Twitter amesema: "Nampongeza Mheshimiwa Magufuli na Chama cha Mapinduzi kwa ushindi wa kishindo katika uchaguzi."

Kwa upande wake, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amempongeza Magufuli kwa ushindi wake na kusema  kuchaguliwa tena Magufuli ni ishara ya upendo na imani  waliyonayo Watanzania kwa uongozi wake.

Rais Magufuli (kushoto) na Rais Kenyatta 

"Kwa niaba ya Watu, Serikali ya Kenya na Mimi mwenyewe nampongeza ndugu yangu, Dkt John Pombe Magufuli kwa ushindi wake na wa Chama Cha Mapinduzi, katika uchaguzi uliomalizika", alisema Rais Kenyatta.

Aliongeza kuandika: ''Nchi ya Kenya inatarajia kuendelea kufanya kazi na utawala wako kwa faida ya watu wa mataifa yetu mawili, kwa ustawi wa Afrika Mashariki na kwa amani, utulivu na ukuaji wa bara la Afrika.

Serikali ya China nayo pia imempongeza Magufuli kwa kuchaguliwa tena huku ikisema ina matumaini kuwa uhusiano baina ya nchi mbili utaimarika zaidi.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Wang Wenbin amesema China inaamini kuwa chini ya uongozi wa Rais Magufuli, Tanzania itaendelea kupiga hatua zaidi za maendeleo.

Hayo yanajiri wakati ambao vyama vya upinzani nchini Tanzania vya CHADEMA na ACT Wazalendo vimesema kuwa havitambui matokeo ya uchaguzi. 

Tags