Nov 03, 2020 07:13 UTC
  • Outtara (78) ashinda muhula tata wa tatu wa urais Ivory Coast kwa 94%

Tume ya Uchaguzi ya Ivory Casot imemtangaza Rais wa sasa wa nchi hiyo, Alassane Ouattara kuwa mshindi wa uchaguzi wa rais uliofanyika Jumamosi iliyopita.

Kwa mujibu wa matokeo hayo ya muda yaliyotangazwa mapema leo Jumanne na Kuibiert-Coulibaly Ibrahime, Mkuu wa Tume ya Uchaguzi Kodivaa, Outtara mwenye umri wa miaka 78 ameibuka mshindi kwa kuzoa asilimia 94 ya kura zilizopigwa.

Amesema idadi ya wapiga kura walioshiriki zoezi hilo la kidemokrasia ambalo lilisusiwa na upinzani ni asilimia 53.9.  Wapinzani wa Ivory Coast walisusia uchaguzi huo wakipinga hatua ya Outtara ya kugombea tena kwa mara ya tatu mfululizo.

Kinachosubiriwa sasa ni tangazo rasmi la Baraza la Katiba, ambalo litamtangaza mshindi wa uchaguzi wa urais wa Oktoba 31, baada ya kusikiliza malalamiko na mapingamizi ya wanaotilia shaka mchakato wa zoezi hilo wakisisitiza kuwa liligubikwa na kasora nyingi.

 

Ghasia za kabla ya uchaguzi Kodivaa

Mwaka 2016 Katiba ya Ivory Coast ilibana kipindi cha mtu kugombea urais. Kwa mujibu wa marekebisho hayo ya katiba, mtu yeyote haruhusiwi kugombea urais kwa zaidi ya mihula miwili ya miaka mitano mitano. Hata hivyo wafuasi wa Ouattara wanasema kuwa, marekebisho ya Katiba ya mwaka 2016 yalifuta yote yaliyopita kabla ya hapo kwa maana kwamba Ouattara anahesabiwa kana kwamba hajawahi kugombea urais hata mara moja. 

Watu wasiopungua 30 wameuawa katika ghasia za kabla ya uchaguzi nchini humo, huku wadadisi wa mambo wakionya kuwa, tangazo la leo la Tume ya Uchaguzi linatazamiwa kuchochea zaidi moto wa machafuko.

Tags