Nov 05, 2020 11:46 UTC
  • Rais Magufuli wa Tanzania aapishwa, atoa mwito wa ushirikiano

Rais John Pombe Magufuli ameapishwa leo Alkhamisi kuhudumu muhula wa pili na wa mwisho wa kuiongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Magufuli ameapishwa na Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma katika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma uliokuwa umefurika wananchi na wageni waalikwa wa ndani na nje ya nchi. Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan naye pia amekula kiapo cha kulitumikia taifa kwa uaminifu.

Akihutubia taifa baada ya kula kiapo, Rais Magufuli amesema uchaguzi mkuu wa Oktoba 28 umekwisha na sasa kinachotakiwa kufanyika ni kujikita katika masuala ya maendeleo.

Aidha ameahidi kuimarisha uhusiano na ushirikiano na nchi rafiki pamoja na taasisi mbalimbali, kama ilivyokuwa katika miaka mitano iliyopita. Rais wa Tanzania ameahidi kuheshimu kiapo cha uongozi alichokula pamoja na makamu wake, bila kujali tofauti za kiitikadi, dini, kabila au rangi.

Ameeleza bayana kuwa, "nitashirikiana nanyi kwa karibu katika kuendeleza jitihada zetu za kujikomboa, na kujenga taifa litakalojitegemea, na katika hilo tunalenga kukamilisha miradi mikubwa tuliyoianzisha na kuleta mingine mipya."

Tundu Lissu, mgombea wa Chadema aliyepinga matokeo ya uchaguzi wa urais

Dakta Magufuli aliibuka mshindi wa kinyang'anyiro cha urais cha Oktoba 28, baada ya kupata kura zaidi ya milioni 12, sawa na asilimia 84.4 ya kura zote halali zilizopigwa, kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Tundu Lissu, mgombea wa chama cha upinzani cha Chadema aliyepata kura karibu milioni 2 alipinga matokeo ya uchaguzi huo, akisisitiza kuwa zoezi hilo liligubikwa na mizengwe na uchakachuaji wa matokeo.

Jumatatu iliyopita, Dakta Hussein Ali Mwinyi aliapishwa kuwa Rais wa nane wa Zanzibar katika hafla kubwa iliyofanyika katika Uwanja wa Amaan visiwani humo, baada ya kushinda uchaguzi wa rais kupitia CCM, na kumbwaga mshindani wake wa karibu, Maalim Seif Shariff Hamad aliyewania kwa tiketi ya ACT-Wazalendo.

Tags