Nov 07, 2020 11:47 UTC
  • Kinara wa upinzani Ivory Coast akamatwa kwa kuunda serikali hasimu

Kiongozi wa upinzani na Waziri Mkuu wa zamani wa Ivory Coast, Pascal Affi N’Guessan amekamatwa na vyombo vya usalama nchini humo kwa kuunda serikali hasimu, siku chache baada ya Tume Huru ya Uchaguzi (CEI) kumtangaza Rais Alassane Ouattara kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika Oktoba 31.

Mke wa N'Guessan, Angeline Kili katika mahojiano na shirika la habari la Reuters, amethibitisha habari za kukamatwa mwanasiasa huyo lakini amesema hajui aliko hivi sasa.

Kadhalika Genevieve Goetzinger, msemaji wa kinara huyo wa chama cha FPI amesema katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa: N'Guessan amekamatwa usiku wa kuamkia leo katika mji wa kusini mashariki wa Akoupe, akiwa njiani kuelekea katika makazi yake yaliyoko mjini Bongouanou.

Waendesha mashitaka nchini humo wameazimia kuwafungulia mashitaka ya 'ugaidi' zaidi ya viongozi 12 wa upinzani waliosusia uchaguzi huo mkuu.

Alassane Outtara

Kwa mujibu wa tume ya uchaguzi, Ouattara aliibuka mshindi wa uchaguzi wa Oktoba 31 kwa kuzoa asilimia 94.27 ya kura huku, Henri Konan Bédié akipata asilimia 1.66, Kouadio Konan Bertin asilimia 1.99 na Pascal Affi N’guessan akipata asilimia 0.99 ya kura zilizopigwa. Tume hiyo imesema kiwango cha ushiriki katika uchaguzi huo ni asilimia 53.90. Matokeo haya yanatarajiwa kuthibitishwa na Mahakama ya Katiba.

Rais Ouattara, 78,  amekuwa madarakani kwa takriban muongo mzima, lakini anadai katiba mpya iliyoidhinishwa mwaka 2016 inamruhusu kugombea tena urais kwa muhula wa tatu.

Tags