Nov 09, 2020 04:34 UTC
  • Mivutano yaongezeka kati ya Morocco na harakati ya Polisario

Mfalme wa Morocco ametuma ujumbe mkali kwa harakati ya Polisario na kueleza kuwa Rabat itakabiliana kwa nguvu na umakini na jitihada zozote zenye lengo la kuvuruga amani ya maeneo ya kusini mwa nchi hiyo.

Katika ujumbe wake huo kwa harakati ya Polisario, Mfalme Mohammed wa Sita wa Morocco ameashiria mivutano ya karibuni katika eneo la mpakani la Guerguerat na kusistiza kuwa Morocco siku zote inachukua hatua kwa mujibu wa mantiki na kwamba itakabiliana kwa nguvu na jitihada zozote zenye lengo la kuvuruga uthabiti wa maeneo ya kusini mwa nchi. 

Mfalme Mohammed wa Sita wa Morocco ameyasema hayo ikiwa ni jibu kwa kitendo cha kusumbuliwa raia wanaotumia kivuko cha mpakani cha Guerguerat kinachopatikana baina ya Morocco na Mauritania. Imebainika kuwa, wahusika wa matukio hayo ni watu wenye mfungamano na harakati ya Polisario. 

Mfalme Mohammed wa Sita wa Morocco 

Mfalme wa Morocco amesisitiza kuwa, nchi yake inafungamana na ushirikiano uliopo kati yake na Umoja wa Mataifa katika fremu ya kuheshimu maazimio ya Baraza la Usalama ili kupata ufumbuzi wa mwisho kwa mujibu wa mpango wa serikali inayojiendeshea masuala yake yenyewe.

Siku kadhaa zilizopita hali ya mvutano imeripotiwa kuongezeka katika eneo la mpakani la Guerguerat sambamba na kufanyika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa cha kuchunguzwa azimio la kuongeza muda wa uwepo wa ujumbe wa umoja huo huko Sahara Magharibi. 

Harakati ya Polisario ni taasisi ya kisiasa na kijeshi ya wananchi wa eneo la Sahara Magharibi huko kaskazini magharibi mwa Afrika na kusini mwa nchi ya Morocco inayopigania kuwa uhuru eneo hilo. 

Tags