Nov 09, 2020 13:00 UTC
  • Godbless Lema
    Godbless Lema

Mwanasiasa maarufu wa upinzani nchini Tanzania Godbless Lema amekamatwa na maafisa wa polisi Kenya baada ya kuingia nchini humo kinyume cha sheria kwa lengo la kuomba hifadhi ya kisaisa.

Kwa mujibu wa gazeti la Standard la nchini Kenya, Lema ambaye alikuwa mbunge wa jimbo la Arusha mjini kwa tiketi ya Chadema amekamatwa Jumapili  akiwa ameambatana na familia yake. Alikuw akielekea jijini Nairobi kwa ajili ya kutafuta makaazi ya muda.

Maafisa wa polisi katika kaunti ya Kajiado nchini Kenya wanasema wanamshikilia Lema na wanapanga kumrejesha Tanzania mwanasiasa huyo ambaye amedai anakandamizwa kisiasa na anahofia maisha yake.

Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limetoa wito kwa serikali ya Kenya kutomrejesha Tanzania mwanasiasa huyo kutokana na kile ambacho limekitaja kuwa ni ukandamizaji wa kisiasa katika nchi hiyo.

Amnesty International imeitaka serikali ya Kenya ifungamane na Mkataba wa Mwaka 1951 wa Wakimbizi ambao unataka nchi zilizosaini mkataba huo kuwapa hifadhi bila masharti wakimbizi na watu waliokandamizwa kisiasa. Mkurugenzi Mtendaji wa Amnesty International nchini Kenya Irungu Houghton amesema Kenya haipaswi kukiuka sheria za kimataifa ambazo zinaizuia kuwafukuza watu ambao wametoroka nchi yao wakihofia ukandamizaji.

Mgombea urais wa Chadema, Tundu Lissu

Lema ambaye alikamatwa na kuachiliwa siku chache zilizopita amewaambia waandishi habari Kenya kuwa amekimbilia Kenya kwa kuhofia maisha yake.

Wakili wa Lema,  George Wajackoyah, ametoa wito kwa polisi kumuachilia huru mteja wake na kumkabidhi wa Shirika la Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Wakimbizi UNHCR. Amesema amezungumza na maafisa wa ngazi za juu serikalini na wanafuatilia kesi hiyo. Aidha amesema familia ya Lema sasa iko mikononi mwa maafisa wa UNHCR mjini Nairobi.

 

Tags